Ratiba ya kuaga mwili wa Akwilina Akwiline, mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) aliyefariki dunia kwa kupigwa risasi Februari 16,2018 itaanza saa tatu asubuhi Alhamisi.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Februari 20,2018 nyumbani kwa dada wa Akwilina, baba mdogo wa marehemu Valentino Akwiline amesema wanatarajia kuusafirisha mwili Alhamisi Februari 22,2018 kuelekea Mashati Olele wilayani Rombo mkoani Kilimanjaro kwa mazishi yatakayofanyika Ijumaa.
Amesema ratiba itaanza saa tatu asubuhi kwa mwili kufikishwa nyumbani kwa Tegolena Uiso ambaye ni dada wa Akwilina ambako kutafanyika ibada.
"Mwili utaondoka Muhimbili saa tatu asubuhi kuja hapa nyumbani, tunatarajia ufike saa tano asubuhi na kutakuwa na misa fupi na chakula kwa watakaohudhuria.”
"Tunatarajia saa saba mwili utaondoka hapa nyumbani kuelekea katika viwanja vya Chuo cha NIT ambako shughuli kubwa ya kuaga mwili zitafanyika. Saa tisa alasiri tutaanza safari kuelekea Rombo," amesema.
Soma: VIDEO-Mazishi ya Akwilina kugharimu Sh80 milioni
Wakati huohuo, msemaji wa familia Festo Kavishe ametoa ufafanuzi kuhusu gharama za mazishi akisema zinaweza kubadilika wakati wowote.
"Sh80 milioni yalikuwa ni makadirio ya mazishi haya, lakini tayari tumeshaikabidhi Serikali mchanganuo huo hivyo tunasubiri taarifa kutoka kwao," amesema Kavishe.