BILA shaka wengi watakuwa wamejaribu kujiuliza, swali hili je ni nani hasa, ana wajibu wa kumtunza mwenzake baina ya wanandoa au kati ya mke na mume?
Ni mwanaume au ni mwanamke ama ni wote kwa pamoja, kila mmoja kwa nafasi yake?
Sheria inasemaje kuhusiana na suala au hoja, hii? Awali ya yote, suala la matunzo kwa wanandoa, lenyewe, liko kwa mujibu wa sheria.
Hivyo ni sawa na kusema kuwa matunzo siyo suala la hisani, zawadi au upendeleo fulani maalum kutoka kwa mume kwa ajili ya mke au mke kwa ajili ya mumewe.
Sheria ya Ndoa ya mwaka 1971 imeweka bayana habari nzima ya matunzo baina ya wanandoa.
Niseme mapema tu kuwa wapo wanaojua kuwa mume peke yake ndiye mwenye wajibu au jukumu la kutoa matunzo kwa mke.
Tena kuna baadhi ya wanawake hujiaminisha kuwa fedha zao si za kutunza familia bali ni za kujipamba na kununua kile wanachotaka kwa vile kazi ya kutunza watoto na yeye mama ni ya baba au mume.
Sivyo hivyo muda wote wakati mwingine mama.
Matunzo ni nini?
Kifungu cha 63(a) cha Sheria ya Ndoa, 1971 kinataja vitu ambavyo kisheria ndivyo vinavyotambulika kama matunzo kwa wanandoa ambao ni mume na mke.
Kifungu hiki kinabainisha bayana kuwa, makazi, mavazi na chakula, haya ndiyo mahitaji ya msingi ambayo, kila, mwanandoa mume au mke mwenye wajibu wa kuyatoa, kwa kuzingatia uwezo na nafasi yake kiuchumi, atatakiwa kuwapa au kuyatimiza kama wajibu wake kwa mwanandoa mwenzake.
Wajibu wa mke kutoa matunzo kwa mume wake.
Ni vema ikafahamika kuwa suala la matunzo linawahusu wanandoa wote yaani mke pamoja na mume.
Kila mmoja anao wajibu kwa mwenzake katika kutoa matunzo. Isipokuwa wajibu wa aina gani kwa nafasi fulani, unatofautiana baina ya hawa wahusika wawili.
Hii ni kutokana na ukweli kwamba, mke na mume wote wanao wajibu unaoambatana na mipaka katika kutoa matunzo yanayowahusu ili ndoa yao idumu.
Kifungu cha 63(b) cha Sheria ya Ndoa, 1971 kinasema kuwa mwanamke au mke ambaye ana uwezo ana wajibu wa kutoa matunzo kwa mume wake ambaye hajiwezi, ambaye ana ugonjwa wa kimwili au kiakili ambao haumuwezeshi kufanya kazi ya kumwingizia kipato.
Hivyo basi, wajibu wa mwanamke au mke kumhudumia mwanaume ambaye ni mume ni pale tu mwanaume huyu anapokuwa amepatwa au kufikwa na ulemavu au ugonjwa wa akili au mwili.
Na kama haitoshi, ugonjwa au ulemavu husika ni lazima uwe ni kwa kiwango cha kutomwezesha mhusika au mume kufanya kazi.
Tofauti na mwongozo huu, dhahiri mlengwa atakuwa nje ya muktadha wa ulinzi au utetezi wa kifungu hicho.
Maana yake ni kuwa, ikiwa mwanaume au ume wa ndoa anajiweza siyo mgonjwa au siyo mlemavu au ni mgonjwa au mlemavu lakini ugonjwa au ulemavu huo haumzuii, kuweza, kufanya kazi ya kujiingizia kipato basi mwanamke au mke wake hatawajibika kumpa matunzo.
Wajibu wa mume kutoa matunzo kwa mke wake, huu unabainishwa katika kifungu cha 63(a) cha sheria hiyo kinachosema kuwa ni wajibu wa mume kumtunza mke wake au wake zake kwa ndoa ya mke zaidi ya mmoja kwa kuwapa makazi, mavazi na chakula kutokana na uwezo wake wa kipato uchumi.
Kwa muktadha wa kifungu hiki hapo juu, utaona tofauti kati ya wajibu wa mwanamke mke katika kutoa matunzo na ule wa mwanaume (mume). Kwa mwanaume au mume wa ndoa kutoa matunzo ni muda wote ndani ya ndoa.
Haijalishi, aidha mke husika ni mlemavu au mgonjwa, ni mzima wa afya; anao uwezo wa kufanya kazi lakini ni mama wa nyumbani, lazima mwanaume (mume) atatoa matunzo.
Jambo la msingi la kuzingatia hapa ni kuwa mwanaume au mume wa ndoa atawajibika kutoa matunzo husika kwa kuzingatia uwezo wake wa kipato au uchumi binafsi.
Haitowezekana kuishawishi mahakama, katika shauri, kuamuru mwanaume au mume kutoa matunzo zaidi kuliko uwezo wa kipato chake na hata kukubaliwa kutoa chini ya kile kiwango kinachowezekana kulingana na uwezo wake.