OFISI ya Uhamiaji Dar es Salaam imesema ilimuita na kumuhoji Kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la soka Tanzania (TFF), Wilfred Kidao, juu ya uraia wake ikiwa ni taratibu za kawaida za ofisi hiyo.
Kidao, jana aliitwa kwenye ofisi hizo kwa kile kilichoelezwa kuhoji uraia wake kufuatia taarifa za chini chini kuwa si raia wa Tanzania.
Akizungumza na redio moja jijini Dar esSalaam jana, Msemaji Mkuu Idara ya Uhamiaji, Ally Mtanda, alisema kuwa idara hiyo inafanya kazi yake kufuatana na sheria za nchi na imemuhoji Kidao katika uratibu wa kawaida wa ofisi hiyo.
"Ni kweli tumemuhoji kutokana na taarifa tulizozipata, na hili ni jambo la kawaida pindi tunapopata taarifa kama hizi, baada ya mahojiano idara inaendelea na taratibu za kazi zake," alisema Mtanda.
Kidao, alipotafutwa na Nipashe kuelezea nini kimepelekea kuhojiwa juu ya uraia wake, alisema 'No comment' akimaanisha hana cha kuongea.
"Kama mtu wa Serikali amesema basi, 'No coment' maana hapo mimi nitaongea nini sasa," alisema Kidao.