Shamrashamra za kuelekea katika tamasha la Sauti za Busara zinazidi kupamba moto Zanzibar, huku wapenzi wa tamasha hilo wakiwa na hamu ya kutaka kujua nani ataanza kutoa burudani.
Tamsaha hilo ambalo litakuwa na zaidi ya wasanii 400 na vikundi vya burudani vipatavyo kundi 40 vya kuchagua, vinatarajiwa kutoa burudani kali katika uwanja wa Ngome Kongwe kisiwani humo.
Zakes Bantwini ni miongoni mwa wasanii wanane wa Afrika Kusini ambao wamewahi kutumbuiza katika tamasha hilo, wengine ni Thandiswa na Kwani Experience. Akiwa na baadhi ya nyimbo zinazotamba kwenye kumbi za starehe, kama vile Clap Your Hands, Wasting My Time, Ghetto na Bang, Bang, Bang ana uhakika wa kuvuta mashabiki kutoka katika kila kona ya Kusini mwa Afrika.
Licha ya kuwahi kufanya maonyesho kadhaa Tanzania, Kidum na Bendi yake ya Bod Boda watatumbuiza kwa mara ya kwanza katika tamasha hilo, huku akiwa na shauku ya kuwaonjesha nyimbo zake mpya akijumuisha na baadhi ya nyimbo zake zinazotamba katika chati za redio mbalimbali, kutoka katika albamu zake sita alizoziachia tangu mwaka 2001.
Akiwa amezaliwa nchini Marekani na wazazi waliotokea katika nchi za Rwanda na Uganda, mwanamuziki mwenye sauti nzuri na mtunzi wa nyimbo, Somi ambaye aliachia kibao chake cha ‘Petite Afrique’ mwaka 2017 nae ni miongoni mwa wasani mahiri barani Africa.
Kwa Saida Kairoli, jukwaa la Sauti za Busara ni sehemu iliyoandaliwa maalumu kwa ajili yake kuja upya kimataifa akiwa ni mmoja wa wanamuziki wanaopendwa Tanzania.
Baada ya kipindi cha muda mrefu kutokuwepo katika tasnia ya burudani, kiu ya mashabiki ilirudishwa mwaka 2017, baada ya mwanamuziki Diamond Platnumz kurudia wimbo maarufu wa Saida Karoli unaoitwa “Maria Salome”.
Kwa mujibu wa Meneja wa Tamasha la Sauti za Busara, Journey Ramadhan, vikundi vyote vilivyochaguliwa katika Tamasha la Busara ni wasanii nyota katika bara la Afrika na kwingineko.
”Mwaka huu orodha ya wasanii itakuwa ‘nzuri sana’ haijawahi kutokea, ndiyo maana hata mchakato wa uchaguzi ulichukua muda kidogo, lakini naweza pia kuelewa kuhusu watu kung’ang’ania aina fulani ya muziki ambao ni chaguo lao linalowakilisha mapenzi yao,” aliongeza Ramadhan.
“Tumeshughulikia idara hiyo na masuala mengine yanayohusiana na idara hiyo ili kuhakikisha kwamba wahudhuriaji wanakutana na uzoefu wenye tija. Uzoefu huu ndiyo jambo ambalo wahudhuriaji wa tamasha wanasubiria kwa hamu bila hivyo basi huwa ni tamasha la kawaida kama mengine tu,” anasema Ramadhan.