Hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam juzi ilitangaza ofa ya chumba cha Sh22.4 milioni katika Usiku wa Valentine na kusema kuwa Watanzania mbalimbali wamekuwa wakipiga simu kutaka kujua kama ni bei halisi na wengine kuomba punguzo.
Hayo yalisemwa na Mkurugenzi wa Masoko na Mauzo, Denis Glibic alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuhusu chumba hicho na namna watu walivyolipokea tangazo hilo.
Glibic alisema tangu watangaze ofa hiyo ambayo ni kwa ajili ya wapendano katika sikukuu ya Valentine, wamepokea simu nyingi kutoka kwa Watanzania wakitaka kujua kama kweli hilo ni tangazo lao halisi na wengine wakitaka wapate nafasi hiyo kwa punguzo la bei.
Kuhusu chumba hicho ambacho kinatumiwa na marais mbalimbali duniani wanapokuja nchini, meneja mwendeshaji wa hoteli hiyo, Timothy Mlay alisema, kwa kawaida bei yake huwa ni Sh11.4 milioni kwa siku.
Alisema pamoja na kuwapo kwa malalamiko ya maisha magumu, wanaamini watu watapatikana kwani kwao kuanzia Desemba mpaka sasa ni kipindi ambacho hupata wateja wengi.
Alisema huduma zitakazotolewa kwa wateja wa chumba hicho siku hiyo zitakuwa tofauti kwa wateja wengine, kwani mbali ya kwenda kuchukuliwa na gari la kifahari eneo wanaloishi, pia watapatiwa zawadi za mapambo ya mwilini yenye madini ya Tanzanite