Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Simon Sirro amewataka askari kuzingatia maadili ya kazi na kuacha kuwabambikia watu kesi, kujiingiza katika vitendo vya rushwa.
Sirro ametoa kauli hiyo jana Februari 21, 2018 katika ziara yake ya siku moja wilaya za Handeni na Korogwe mkoani Tanga, ambako licha ya mambo mengine alikagua majalada ya kesi, vielelezo na kuzungumza na askari kuhusu nidhamu.
Amesema askari atakayebainika kupokea rushwa na kuwabambikia watu kesi atachukuliwa hatua za nidhamu.
“Ninatembelea vituo vya polisi kukagua majalada ya kesi, kuangalia sababu za kesi kuchelewa. Pia, ninaangalia kama kuna kesi ambazo wahusika wamebambikiwa ili kuyafanyia kazi mambo haya,” amesema Sirro.
Pia, amevitaka vyombo vya dola Tanga kutoa elimu dhidi ya kesi za ubakaji na wizi wa mifugo kwa kuwa zinaonekana kukithiri na kutaka hatua stahiki zishukuliwe kwa wahusika.
“Kama kuna kubambikia watu kesi tutabaini, tukimbaini askari tutamwajibisha ndiyo maana ninapitia majalada na vielelezo kuona wanakwama wapi ili tujue kama tatizo ni ofisi ya mkemia mkuu, waseme ili tuweze kufuatilia na kumaliza hizi kesi kwa kutenda haki,” amesema.