Akizungumza na watumishi walio chini ya Msajili wa Mahakama ya Wilaya ya Tabora mjini hapa juzi, jaji mkuu aliwataka watumishi wa mahakama kuwa na tabia ya kuwapa elimu wananchi kuhusiana na haki zao.
Alieleza kuwa wananchi wengi hawajui haki zao na elimu kuhusu haki zao itawasaidia. “Haki huanza kwa usuluhishi, mahakama inapaswa kuwaongoza na kuwaelimisha wananchi ili wajue kuwa ni sehemu ya kupata haki na si vinginevyo,” alisema.
Akizungumzia ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Sikonge, alisema utakamilika mwaka huu na kuanza kazi mara moja. Hadi sasa Sikonge haina mahakama ya wilaya na inategemea ile ya Tabora na wananchi hutumia muda na pesa nyingi kufuata haki zao mjini humo.
Aliongeza kuwa wakati wakisubiri ujenzi wa Mahakama ya Wilaya ya Uyui yenye mahakama moja, tena ya mwanzo wanajipanga kutumia mahakama zinazotembea kuwapunguzia mzigo wananchi wa maeneo yasiyo na mahakama.
Awali, akizungumza na sekretarieti ya Mkoa wa Tabora, Profesa Juma aliyataka mabaraza ya kata yatekeleze majukumu yake kwa kuzingatia sheria ili kuwapunguzia watendaji wa Serikali malalamiko. Jaji mkuu aliongeza kuwa mabaraza hayo ambayo yalianzishwa kwa matakwa ya Katiba ya nchi kazi yake ni usuluhishi na ndiyo maana hata adhabu zake ni ndogo.
Alimuelekeza Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Aggrey Mwanri kufuatilia kwa ukaribu utendaji kazi wa mabaraza hayo kwa kuwa ndiyo yamekuwa chanzo cha migogoro ya ardhi na mashauri ya mirathi.
Akizungumza katika mkutano huo, Mwanri alisema ofisi yake hupokea malalamiko yanayohusiana na ucheleweshaji wa majalada ya hukumu.