Mwenyekiti Kamati ya muda ya uongozi wa CUF, Julius Mtatiro amesema hata kama angelikuwa ni miongoni mwa wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) asingeweza kukubali kukitumikia cheo cha Humphrey Polepole kwa madai sio kazi sahihi.
Mtatiro ametoa kauli hiyo mapema leo asubuhi katika ukurasa wake wa kijamii baada ya kupita masaa kadhaa tokea Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Humphrey Polepole kuongea na waandishi wa habari na kuwataka vyama vya upinzani viwe na uvumilivu katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika kesho (Jumamosi) kwa sababu ni kawaida yao kushindwa katika chaguzi zote.
"Hata kama ningelikuwa mwana CCM, ningeikataa kazi ya usemaji wa CCM. Ina hukumu nyingi sana mbeleni, si kazi sahihi", ameandika Mtatiro.
Kwa upande mwingine, Kesho (Jumamosi) Wananchi wa Jimbo la Kinondoni, Siha wanatarajia kuingia katika zoezi la kupiga kura ili waweze kumpata muwakilishi mmoja katika jimbo lao aweze kwenda kuwatetea maslahi yao ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linalotarajiwa kuanza Aprili 03 mwaka 2018.