Kesi za Madai ya Talaka Zazidi Kuongezeka

Kesi za Madai ya Talaka Zazidi Kuongezeka
Kesi 1,218 za madai ya talaka visiwani Zanzibar zimeripotiwa katika mahakama mbalimbali za kadhi kuanzia Januari hadi Desemba, 2017.

Naibu Waziri wa Nchi Afisi ya Rais, Katiba, Sheria na Utumishi wa Umma na Utawala bora, Khamis Juma Maalim amesema hayo leo Februari 13, 2018 katika kikao cha Baraza la Wawakilishi wakati akijibu swali la mwakilishi wa Konde, Omar Seif Abeid.

Katika swali lake, Abeid alihoji sababu za ndoa nyingi hasa za vijana kudumu muda fupi, huku akitaka kujua katika kipindi cha mwaka 2017 ni madai mangapi ya ndoa yamefikishwa katika mahakama ya kadhi ili kupatiwa ufumbuzi.

Katika majibu yake Maalim amesema kiwango cha kesi hizo ni nyingi ukilinganisha na mwaka 2016 ambapo kulikuwa na kesi 1,000.

Amesema katika kesi za mwaka 2017,  kesi 884 ziliripotiwa katika mahakama za kadhi za Unguja,  440 zimetolewa uamuzi na 444 bado zinaendelea kusikilizwa katika mahakama hizo kwa hatua zaidi za kisheria.

Amesema kwa upande wa Pemba, kulikuwa na  kesi 334, kati ya hizo 249 zimetolewa uamuzi huku 85 zikiendelea kusikilizwa.

Kuhusu sababu za ndoa kuvunjika katika kipindi cha muda mfupi sambamba na kuwekwa sheria ya kuzuia utoaji talaka, Maalim amesema swali hilo ni zuri lakini ni ngumu kwa sababu jambo hilo litakwenda kinyume na maadili ya Wazanzibar walio wengi ambao ni Waislam.

“Kama tunavyoelewa wananchi wengi wa Zanzibar ni Waislam ni wazi kuwa kuandaa kwa Sheria kama hiyo ni kwenda kinyume na Sheria zilizowekwa na dini ya kiislam,” amesema,

“Hatuna utafiti ambao unaonyesha kuwa kati ya mwanamke na mwanaume nani ni sababu ya kutoka kwa talaka hovyo ijapokuwa suala la talaka ni la siku nyingi.”

Amesema kazi kubwa inayofanywa na wizara yake kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ni utoaji wa elimu juu ya kuishi vema katika maisha ya ndoa, lengo ni kuona suala la talaka linapungua kwa kiasi kikubwa.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad