Kitambulisho cha Taifa Kimekua Dili


Kitambulisho cha Taifa Kimekua Dili
Kati ya vitu muhimu ambavyo mwananchi yeyote anapaswa kuwa navyo kwa sasa ni Kitambulisho cha Taifa.

Umuhimu huo hautokani na kumtambulisha mwananchi kuwa ni raia wa Tanzania tu, bali sasa ndicho kitakachomuwezesha kusajili kampuni, kuomba hati ya kusafiria na kupata cheti cha kuzaliwa.

Kitambulisho hicho kinachotolewa na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida), ni mkakati wa Serikali kuhakikisha kuwa kila Mtanzania mwenye miaka 18 na kuendelea anakuwa nacho ili kumwezesha kupata huduma muhimu.

Januari 31, Kamishna Jenerali wa Idara ya Uhamiaji, Dk Anna Makakala alisema ili Mtanzania apate hati ya kusafiria ni lazima awe na Kitambulisho cha Taifa na si vinginevyo.

Wakati Uhamiaji ikisisitiza kitambulisho hicho, jana Wakala wa Usajili wa Kampuni (Brela) ulitangaza kuanza kusajili kampuni kwa njia ya mtandao huku kigezo kikuu ili kusajili kikiwa Kitambulisho cha Taifa.

Taarifa ya Brela iliyotolewa jana inasema ambao hawajasajiliwa kupata vitambulisho, wataendelea kusajiliwa kwenye ofisi za Nida.

Juzi, Wakala wa Usajili, Udhamini na Ufilisi (Rita) ulisema kuanzia sasa, wananchi wanaweza kutumia Kitambulisho cha Taifa na cha kupiga kura kupata cheti cha kuzaliwa.

Baadhi ya mambo muhimu kuhusu kitambulisho hicho ni kusaidia kuongeza wigo wa mapato ya Serikali, kumtambua mhusika kirahisi anapohitaji kupatiwa huduma katika taasisi mbalimbali kama vile benki, taasisi za mikopo na huduma za afya.

Pia, vitarahisisha kuwatambua wakwepaji wa kurejesha mikopo kutoka kwenye benki na asasi mbalimbali za fedha nchini, kuweka kumbukumbu za matukio ya uhalifu katika daftari la kumbukumbu la kielektroniki.

Kitambulisho hicho kitawezesha pia kumtambua mtu anapofanya biashara au shughuli nyingine kwa kutumia majina tofauti. Vitahakikisha kuwa mtu anapata stahili zake za jamii.

Kwa mfano, kupata malipo ya pensheni, haki za matibabu, haki za kujiunga na masomo ikiwa ni pamoja na stahili zozote ambazo raia wa Tanzania anastahili kupata kirahisi kwani kupitia Kitambulisho cha Taifa, mwananchi atatambulika kirahisi (nani ni nani, yuko wapi na anafanya nini.

Umuhimu mwingine ni kuondoa watumishi hewa kwenye mfumo wa malipo ya mishahara ‘payroll’ ya Serikali, kuimarisha utendaji kazi serikalini kwa kuwa na kumbukumbu sahihi za watumishi na malipo ya stahili zao, hasa pale wanapostaafu.

Pia, vitarahisisha kazi ya kuhesabu watu (sensa), kurahisisha kazi ya kuhuisha daftari la wapigakura, kazi ambayo kwa sasa hufanyika mara mbili kabla ya uchaguzi mkuu.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad