Lipumba Kukutana na Viongozi wa CUF Zanzibar
0
February 24, 2018
Mwenyekiti wa CUF anayetambuliwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Profesa Ibrahim Lipumba leo Februari 24, 2018 ameanza ziara Zanzibar na atakutana na kufanya mazungumzo na viongozi mbalimbali wa chama hicho.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF- Bara upande unaomuunga mkono Profesa Lipumba, Magdalena Sakaya ameieleza MCL-Digital leo Jumamosi Februari 24, 2018 kuwa:
“Ziara inaweza kuwa ya siku moja au mbili, akimaliza atarejea Dar es Salaam.”
“Katika ziara hii Profesa Lipumba atakutana na viongozi wa CUF wa Pemba na Unguja kwa lengo la kuimarisha chama.”
Leo saa 4 asubuhi Lipumba alitarajiwa kufanya mkutano katika ukumbi wa Makonyo uliopo Chakechake, Mkoa wa Kusini Pemba.
Wakati Sakaya akieleza hayo, Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar upande unaomuunga mkono Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad, Nassor Ahmed Mazrui amesema hawatambui ziara hiyo kwa maelezo kuwa Profesa Lipumba si kiongozi wao.
“Chama kinawataka wanachama, viongozi na wapenzi wa CUF waliopo Pemba na Unguja kuwa watulivu na kuendelea na shughuli zao za maisha ya kawaida na kupuuza kabisa ujio huo wa Profesa Lipumba,” amesema Mazrui.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kusini Pemba, Shekhan Mohamed Shekhan amesema ana taarifa kamili ya ujio wa kiongozi huyo.
"Ni kweli tumepokea taarifa ya ujio wake na tutatoa ulinzi kwa maana anatambuliwa na vyombo husika kama kiongozi, ukizingatia zaidi mazingira walionayo kwenye chama chao,” amesema.
Tags