Ofisa Msaidizi wa Forodha wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Jennifer Mushi amekana kumiliki magari 19 yenye thamani ya Shilingi Milioni 197,601,207 yasiyolingana na kipato chake katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Mushi amekana umiliki huo, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi wakati akisomewa maelezo ya awali (Ph) na Wakili wa Serikali, Vitalis Peter.
Katika usomewaji wa maelezo hayo, Mushi alikubali majukumu yake ambayo ni kufanya upembuzi na uhakiki wa makadirio ya kodi na bidhaa zinazoingia nchini na kusafirishwa nje ya nchi ambapo alipoajiriwa mwaka 2011 mshahara wake ulikuwa Shilingi Laki nane na mwaka 2016 ulifikia shilingi Milioni 1,190,700.
Wakili Vitalis amedai kwa kipindi chote July 2011 hadi March 2016 mshtakiwa alijipatia kipato cha jumla ya shilingi Milioni 56.7 kama mshahara na marupurupu, ambapo Mushi alikataa.
Mushi alikataa kumiliki magari 19 ambayo anadaiwa aliyaingiza nchini kutokea Japan yakiwa na thamani ya shilingi Milioni 197,601, 207.
Magari hayo ni, Toyota Ra4, Toyota dyna truck, Toyota viz, Suzuki Carry, Toyota ipsum, toyota wish, Toyota mark ll, Toyota regiusage, Toyota estima, Toyota Alex, Toyota Noah, Toyota crown, Toyota hiace, Toyota estima, Toyota passo, Suzuki carry, yote yakiwa na thamani ya Shilingi Milioni 197,601,207
Wakili Vitalis amedai kuwa mshtakiwa anamiliki ardhi au viwanja alivyovinunua kwa nyakati tofauti akiwa mtumishi wa TRA plot namba 2263 block b kimbiji kigamboni chenye thamani ya Milioni 8,400,000 huku shamba la Mabwepande heka moja lenye thamani ya Shilingi Milioni 7.
Pia mshtakiwa huyo alikataa kuwa July 2011 na March 2016 alifanya miamala ya jumla ya shilingi Milioni 310,993,647.33. Pia alikataa kati ya March 2, 2012 na Match 30, 2016 kwenye namba ya simu alifanya miamala wa shilingi 1,632,915, 485.
Katika maelezo hayo, mshtakiwa alikubali kwamba anamiliki shule mbili za awali ambazo ni active tot’s zone maeneo ya Kinyerezi na Mikocheni Dar es Salaam zilizosajiliwa mwaka 2014 na 2016 lakini amekataa kuwa shule hizo zina thamani Milioni 65,063,751.11
Wakili Peter amedai kuwa fedha hizo na mali anazomiliki mshtakiwa hazilingani na kipato chake halali na hivyo hawezi kuelezea utajiri aliokuwa nao.
Baada ya kusikiliza maelezo hayo, Hakimu Shahidi aliahirisha kesi hiyo hadi March 12,2018 kwaajili ya kusikilizwa.