Mzee Kingunge Ngombale Mwiru na mkewe, Mama Peras Kingunge enzi za ujana wao. Mzee Kingunge aliyekuwa mtumishi wa umma kwa zaidi ya miaka 50 amefariki dunia alfajiri ya Februari 2, 2018 akitanguliwa na Mama Peras aliyefariki Januari 4, 2018. Picha kwa hisani ya Familia ya Kingunge Ngombale Mwiru
Miaka michache iliopita, wakati somo wangu katika uandishi wa habari, hayati C. Stanley Kamana, alipofariki dunia, mmoja wa maswahiba wake, James Shani Mpinga, aliandika taazia kwa lugha ya Kiingereza aloipa jina “The Last Sub is no More”.
Neno sub hapo ni kifupisho cha neno sub editor. Katika vyumba vya habari, sub editor ni mtu muhimu maana yeye ndiye anayepitia habari na kuifanyia kazi kikamilifu kabla ya kwenda mtamboni.
Mpinga aliamini kwamba Kamana hakuwa na mfanowe katika eneo hilo hapa nchini. Wakati nataka kuandika kuhusu mzee Kingunge, nimekumbuka kuhusu kichwa cha habari cha Mpinga.
Nataka kusema mzee Kingunge pengine ndiye mwitikadi (Ideologue) wa aina yake wa mwisho kuwepo hapa Tanzania. Hakutakuwa na mwingine kama yeye. Na hatujawahi kuwa naye kabla yake.
Lakini, mwitikadi ni nani?
Mwitikadi ni tafsiri ya lugha ya Kiswahili ya neno lenye asili ya Kifaransa-IDEOLOGUE. Neno hili wala halikuwepo kwenye kamusi ya Kifaransa hadi kwenye karne ya 19. Ni neno jipya.
Hata hivyo, unaweza kulichambua pia katika Kiyunani na ukapata maneno mawili tofauti; Ideo-Hoja, Mawazo na Logos-usomi, uchambuzi.
Kwenye Kiswahili cha kawaida, unaweza kusema ideology ni somo la uchambuzi wa hoja kisayansi na mwitikadi ndiye hasa mtu anayefanya kazi hiyo.
Huyu ni mtu ambaye anayaweka maisha yake ya kisiasa katika kusoma na kubungua bongo yake kwa maslahi ya chama chake na taifa.
Mwenyekiti Mao alijua umuhimu wa kundi la waitikadi ndani ya chama na ndiye aliyekuwa mwanasiasa wa kwanza kuweka mgawanyo huu wa dhahiri kati ya watendaji na waitikadi.
Kazi ya waitikadi ni kusambaza sera na kutoa mwelekeo wa chama. Hawa si watu wa kuwapa mashirika waongoze au kuwa marais. Hawa ni watu wa kutoa miongozo. Kufikiri.
Chama cha Kikomunisti cha China kilikuwa na Lin Biao huku kile cha Urusi kikiwa na Leon Trotsky na baadaye Susilov.
Chama cha Congress cha Milton Obote wa Uganda kilikuwa na Yoga Adholu ambaye yu hai hadi leo.
Kwenye siku zake za mwisho wa utumishi, watu walikuwa wanahoji hivi huyu Kingunge amefanya lipi hasa maana? Walidhani kipimo cha utendaji wa gwiji huyu ni idadi ya majipu alotumbua, wahujumu uchumi aliowakama au miradi aloileta.
Hasha. Mwitikadi anapimwa kwa kukiweka chama chake madarakani, kwa kutengeneza wanasiasa wapya na kwa kuleta mawazo mapya.
Akiwa Mjamaa kindakindaki, Kingunge aliweza kukaa kwenye kamati moja ya mabepari maarufu kama Reginald Mengi na Iddi Simba kutengeneza mwelekeo wa sera mpya za CCM.
Kingunge alikubaliana na mawazo ya watu wenye mtazamo tofauti kama yakiwa na msingi.
Hii ni kwa sababu, kwa mwitikadi, jambo la msingi ni namna mchakato wa hoja ulivyoenda hadi kufikia kwenye uamuzi wa mwisho.
Bahati mbaya ya kizazi chetu ni kwamba waitikadi hawaonekani kuwa wa maana tena. Vyama vimetelekeza utaratibu wa kutengeneza vijana wa kuwa kama akina Kingunge.
Mzee Ngombale hakuibuka tu kama uyoga, kama ilivyokuwa kwa akina Biao, Susilov na Adholu. Watu wa namna hii wanatengenezwa.
Tatizo ni kwamba siku hizi kila kitu ni fasta fasta. Hata ubunge umekuwa ni wa fasta fasta tu. Manake leo mbunge wa Chadema au CUF anahamia CCM na kuwania ubunge bila kupitia mchakato wa kuivishwa kwenye itikadi.
Mwaka juzi, yupo mgombea wa upinzani aliyepanda jukwaani na kusema CCM Hoyee.
Nasubiri kusikia mgombea wa CCM Kinondoni akiwasalimu wananchi kwa kuwaambia Hakii!!!
Hakuna tena itikadi. Ni shaghalabahala. Pengine ndiyo maana Mwenyezi Mungu kaamua kumchukua mzee wa watu.
Pumzika kwa im