Polisi Zanzibar wamezingira makao makuu ya ofisi ya CUF kwa maelezo kuwa wamepata taarifa kwamba kuna mpango wa uvamizi.
Hata hivyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya CUF, Julius Mtatiro ameandika katika ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Facebook kwamba polisi wana ajenda mbili; kuishikilia kimabavu ofisi hiyo au kuweka vitu vya hatari na kisha kuwakamata viongozi wa chama hicho.
Akizungumza na MCL Digital, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Hassan Nassir Ali amethibitisha polisi kulizunguka jengo hilo.
“Ni kweli tumeliweka chini ya ulinzi, kwanza ni kwa sababu kuna viashiria vya watu kufanya uhalifu katika ofisi ya CUF ya Mtendeni tumeweka ulinzi kwanza,” amesema.
“Hatua ya pili tunataka kuingia ndani ili kuthibitisha maneno yanayosemwa ili kama ni kweli tujue tunakabiliana vipi.”
Katika maelezo yake Mtatiro amesema, “Polisi wakiwa na magari kadhaa, wameivamia makao makuu ya CUF Mtendeni, Zanzibar saa 12:10 jioni hii. Inaonekana na inahisiwa wana ajenda mbili.”
“Moja ni kuikalia makao makuu hiyo kimabavu ili kesho Jumatatu waikabidhi kwa bwana yule ili kutekeleza mkakati maalum, au wana lengo la kuingia kimabavu na kuweka vitu hatari na kisha kuwakamata viongozi wa CUF na kudai walitunza vitu hatari ofisini hapo. Tunafuatilia jambo hili kwa ukaribu.”