Mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Mhe Paul Makonda ametoa onyo kali kwa kampuni zinazofanya kazi ya kukamata Pikipiki (bodaboda) kwa mtindo wa kuvamia kitendo kinachohatarisha usalama wa Dereva na Abiria.
RC Makonda amesema zipo baadhi ya kampuni zimekuwa zikivizia madereva wa Bodaboda kisha kuwavamia na kuwakamata na wakati huohuo kuwapiga kitendo ambacho amesema hawezi kukiruhusu kiendelee kwenye Mkoa wake.
Mhe. Makonda ametoa onyo hilo wakati wa kikao na Madalali wanaotekeleza hukumu za Mahakama na Bank kilicholenga kuwatambua na kupitia nyaraka zinazowapa mamlaka ya kufanya kazi hiyo ili Wasionekane Matapeli na waweze kupata ushirikiano wa serikali.
Uamuzi wa RC Makonda kukutana na madalali hao ni manyanyaso na ukandamizaji unaofanywa na baadhi ya madalali wanaopiga minada Nyumba, Magari, Viwanja, Mashamba, Ofisi na Mali za watu bila kufuata taratibu na kusababisha maumivu makali kwa wananchi.
Amesema zipo kampuni za udalali zinazofoji nakala za hukumu, mihuri, sahihi za mahakama,ofisi ya Mkoa, Wilaya na Mitaa na wakati mwingine kufanya minada bila kufuata taratibu.
Baadhi ya wamiliki wa kampuni za udalali
Kutokana na hilo RC Makonda amezitaka kampuni zote za udalali Dar es salaam kuwasilisha nakala za nyaraka ya usajili kwa mwanasheria wa mkoa zipitiwe na kujiridhisha ili wapewe ushirikiano na Serikali.
Nao Madalali wamemshukuru RC Makonda kwa uamuzi wa kuwatambua ili wapate ushirikiano wa Serikali kwakuwa wapo baadhi ya madalali waliokuwa wakifanya kazi hiyo kinyume na sheria na kuwachafulia kazi wale wenaofata taratibu za kazi hiyo.