Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan leo anatarajiwa kuzindua mradi wa kusimamia maliasili na kuendeleza utalii wa kanda ya kusini ujulikanao kama REGROW (Resilient Natural Resource for Tourism and Growth).
Mh. Suluhu anazindua mradi huo wenye lengo la kuongeza mchango wa sekta ya maliasili na utalii katika uchumi wa taifa kwa kuboresha vivutio vya utalii, miundombinu, usimamizi wa vivutio na kuongeza faida za kiuchumi kwa jamii zinazoishi jirani na maeneo ya hifadhi.
Mradi huu ambao maandalizi yake yalianza mwezi Novemba 2014 utazinduliwa rasmi katika viwanja vya Kihesa Kilolo Mjini Iringa ambapo Kauli Mbiu ya uzinduzi huo ni “Utalii kwa Maendeleo Endelevu- Karibu Kusini”.
Taasisi zitakazohusika na utekelezaji wa mradi huo ni Wizara ya Maliasili na Utalii, Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania, Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania, Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Ofisi ya Bonde la Mto Rufiji, Bodi ya Utalii Tanzania, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania kwa kushirikiana na Halmashauri za Wilaya mbalimbali nchini.