Marekani na Urusi zimetoa taarifa kwa nyakati tofauti zikisema zimefikia lengo muhimu la kudhibiti silaha za nyuklia, baada ya kuongezeka wasiwasi kuhusu wajibu wao katika upunguzaji wa silaha hizo.
Mataifa mawili hayo yanayoongoza kuwa na silaha nyingi za nyuklia yamethibitisha kuwa yanaendelea kutekeleza Mkataba Mpya wa START (Strategic Arms Reduction Treaty) ambao ulianza kufanya kazi mwaka 2011.
Makubaliano hayo ya pande mbili yanazitaka kila nchi kuwa na vichwa vya nyuklia chini ya 1,550, na unazilazimisha kupunguza makombora na ndege za kivita. Jumatatu ilikuwa siku ya mwisho ya kuthibitisha utekelezaji wa mkataba huo.
Wakati Marekani imesema imepunguza vichwa vyake vya nyuklia vilivyosambazwa maeneo mbalimbali duniani hadi 1,393, Urusi imeeleza kuwa imepunguza idadi ya silaha hizo hadi 1,444.
Hata hivyo Urusi imekuwa ikiimarisha silaha zake za nyuklia zitumikazo kwenye masafa mafupi ambazo hazipo kwenye mkataba huo.
Rais wa Marekani Donald Trump wiki iliyopita aliutangaza mkakati wa nyuklia wa utawala wake akisema unataka kuimarishwa kwa uwezo wa kujilinda ili kukabiliana na Urusi na nchi nyingine zinazojiimarisha kijeshi.
Watalaam wa kupunguza silaha wanaonya kuwa dunia huenda inarejea kwenye zama za Vita Baridi wakati ambapo hali ya wasiwasi ilikuwa juu kati ya Marekani na Urusi.