Marekani Yamshutumu Odinga kwa 'Kujiapisha' Kenya

Marekani Yamshutumu Odinga kwa 'Kujiapisha' Kenya
Serikali ya Marekani imesema imesikitishwa na hatua ya kiongozi wa upinznai nchini Kenya Raila Odinga ya kujiapisha Jumanne wiki hii.

Marekani pia imeishutumu serikali kwa kufungia vituo vinne vya habari nchini humo ambavyo viliadhibiwa baada ya kupeperusha moja kwa moja hafla hiyo ya upinzani.

Kupitia taarifa, wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema taifa hilo linaamini mizozo yoyote ile inafaa kutatuliwa kwa njia zifaazo kisheria.

"Tunakataa vitendo vyovyote ambavyo vinahujumu Katiba ya Kenya na utawala wa sheria. Uhuru Kenya alichaguliwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Kenya mnamo Oktoba 26, 2017 katika uchaguzi ambao uliidhinishwa na Mahakama ya Juu," taarifa hiyo iliyotumwa na msemaji wa wizara hiyo Hearther Nauerth imesema.

Bw Odinga alisusia uchaguzi huo wa marudio na amesema hamtambui Rais Kenyatta kama rais halali wa taifa hilo.

Jumanne, alikula kiapo kuwa Rais wa Wananchi katika hafla iliyohudhuriwa na maelfu ya wafuasi wake uwanja wa Uhuru Park, Nairobi.

Mgombea mwenza wake Kalonzo Musyoka, ambaye ni makamu wa rais wa zamani, hakuhudhuria sherehe hiyo ingawa walikuwa wameahidi kuapishwa wote wawili kwa pamoja.

Wafuasi wa Bw Odinga wakisherehekea Kisumu baada yake kula kiapo Uhuru Park, Nairobi
Image caption
Wafuasi wa Bw Odinga wakisherehekea Kisumu baada yake kula kiapo Uhuru Park, Nairobi
Bw Musyoka baadaye alisema alipokonywa walinzi wake na hivyo kuzuiwa kuondoka nyumbani kwake kwenda kuhudhuria sherehe hiyo.

Jumatano, mbunge wa upinzani Tom Joseph Kajwang' anayewakilisha eneo bunge la Ruaraka, Nairobi alikamatwa na akashtakiwa kwa makosa ya kuhudhuria mkutano haramu na kushiriki katika kulishwa kiapo kwa Bw Odinga kwa njia ya kudai kumfunga Bw Odinga "kutekeleza kosa la jinai la uhaini".

Bw Kajwang', ambaye ni wakili, alikuwa amevalia sare za uwakili na kwa pamoja na mshauri wa zamani wa Bw Odinga, Miguna Miguna, walikuwa karibu na Bw Odinga alipokuwa anakula kiapo.

Marekani imesema imesikitishwa sana na vitendo vya serikali kwa "kufunga, kutisha na kuminya vyombo vya habari".

"Uhuru wa kujieleza, ikiwa ni pamoja na kwa wanahabari, ni muhimu sana kwa demokrasia, na umelindwa kwenye Katiba ya Kenya," taarifa ya Marekani imesema.

"Tunaihimiza serikali na Wakenya wote kuheshimu uhuru wa kujieleza na kutii agizo la mahakama na kuvifungulia vituo hivyo vya televisheni."

Mahakama ilikuwa imeamuru vituo hivyo vya Citizen, Inooro, NTV na KTN vifunguliwe Alhamisi lakini kufikia Ijumaa asubuhi, agizo hilo lilikuwa bado halijatekelezwa.

Ingawa Marekani imewasifu polisi na vikosi vya usalama kwa jinsi walivyosimamia hafla hiyo ya kuapishwa kwa Bw Odinga Jumanne, wamesema visa vya kukamatwa na kushtakiwa kwa washukiwa vinafaa kutekelezwa kwa kufuata sheria kikamilifu.

Marekani imewahimiza viongozi wa kisiasa Kenya kufanya mazungumzo kwa lengo la kuimarisha uwiano na utangamano na kutatua matatizo ya muda mrefu nchini humo.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad