Msanii Agnes Gerald maarufu Masogange anayekabiliwa na kutumia kutumia dawa za kulevya amesimulia tukio zima namna alivyokamatwa, huku Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ikipanga Februari 21 kutoa hukumu.
Akiongozwa na mawakili Nehemiah Nkoko na Ruben Simwanza kutoa utetezi wake jana, Masogange aliiomba mahakama hiyo imuachie huru kwa sababu hana kosa lolote.
Masogange anakabiliwa na kesi ya kutumia dawa za kulevya aina ya Heroin na Oxazepam, katika utetezi wake alidai kuwa hajawahi kutumia dawa za kulevya hata siku moja. Aliiambia mahakama kuwa mbali ya usanii, alikuwa ni mfanyabiashara wa nguo. Alieleza kuwa Februari 14, 2017 polisi walikwenda nyumbani kwake bila yeye kuwapo kwa sababu alikuwa amempeleka mjomba wake duka la Ocadeco kununua vitu, hivyo walimkuta dada yake.
Aliongeza kuwa polisi hao walimweka dada yake chini ya ulinzi na kumtaka ampigie simu na kujifanye anaumwa ili arudi nyumbani, hivyo alitii amri na baada ya kumjulisha hivyo alimuahidi kuwa atarejea nyumbani punde lakini alirudi saa 12:00 jioni.
Aliendelea kuwa alipofika nyumbani kwake getini kabla hajashuka kwenye gari, alimuona mlinzi amekaa na watu wanne, aliwasalimia na kuingia ndani lakini ilipoingia ndani alimkuta dada yake, askari wa kike na wengine wawili wa kiume, walijitambulisha kwake na kumweleza kuwa wanamsubiri.
Masogange alidai aliwauliza shida yao na walimjibu kuwa wamekwenda kufanya upekuzi, lakini hawajapata kitu chochote.
Baada ya upekuzi huo, walimpeleka Kituo Kikuu cha Polisi na walipofika mapokezi akaandikisha jina na wakampeleka rumande ambako alikaa siku tisa.
Aliongeza kuwa baada ya kukamatwa Februari 14,2017, siku iliyofuatia akiwa polisi alipelekwa ofisi iliyokuwa na watu 15 ambako kwa nyakati tofauti alikuwa wakimuuliza maswali.
Baada ya kufunga ushahidi wake, hakimu mkazi mkuu, Wilbard Mashauri alisema atatoa hukumu Februari 21.