Mbowe Aitaka Serikali Kudhibiti Matukio ya Mauaji ya Kikatili

Mbowe Aitaka Serikali Kudhibiti Matukio ya Mauaji ya Kikatili

Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema Tanzania haitakuwa salama kama haki haitatendeka kwa Serikali kutafuta ufumbuzi na kudhibiti matukio ya watu kuuawa kikatili.

Akizungumza jana wakati wa kuaga mwili wa aliyekuwa Diwani wa Namwawala wilayani Kilombero, Godfrey Luena aliyeuawa Februari 22 kwa kukatwa mapanga, Mbowe alisema Watanzania wasikubali kuingia katika uadui wa kisiasa.

Mbowe alisema matukio yanayotokea sasa ya mauaji yanatia shaka na Serikali isipoyadhibiti itasababisha wananchi wanaopotelewa na ndugu kukaa na manung’uniko.

Alimuomba Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, James Ihunyo aliyehudhuria mazishi hayo kuwatuliza vijana wenye jazba kuhusu matukio yanayoendelea nchini. Mkuu wa Wilaya, Ihunyo aliposimama kuzungumza alisema wameshaunda timu maalumu kuwasaka waliohusika na tukio hilo.

Awali, Mbowe alisema matukio ya mauaji ya kikatili dhidi ya viongozi wa Chadema hayatairudisha nyuma badala yake wataendelea kuimarika.

Alisema kwa kuwa Polisi imetoa tamko kuwa kushambuliwa Luena kunatokana na kisasi, hivyo inawajua watuhumiwa, ana imani watakamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya dola.

Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu alisema ndani ya mwezi mmoja chama hicho kimepoteza viongozi wawili katika matukio yanayofanana. Alimtaja mwingine kuwa ni Katibu wa Chadema Kata ya Hananasif jijini Dar es Salaam, Daniel John ambaye mwili wake uliokotwa katika ufukwe wa Coco.

Mazishi hayo pia yalihudhuriwa na wabunge wa Kilombero Peter Lijuakali, Susan Kiwanga wa Mlimba na Devotha Minja wa Viti Maalumu.
Tags

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Kama vile una uhakika kuwa marehemu aliuawa kwa sababu za kisiasa, acheni kuoanisha kila tukio na siasa, huo ni umbumbumbu uliokengeuka. Pata ukweli kwanza,usitoe majibu mepesi kwa masuala mazito kama hayo. Mbona watanzania wengi yanawasibu hayo, likitokea kwa mwanasiasa, sababu zinakuwa za kisiasa? sijui kwa nini hiki chama kisifutiliwe huko, kila kukicha uchochezi tu, hivi mtapata nini jamii yetu ikihasimiana.

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad