Mbunge Zanzibar Kuwachongea TFF kwa FIFA

Mbunge Zanzibar Kuwachongea TFF kwa FIFA
Siku moja kabla ya ujio wa ujumbe wa Fifa nchini Mbunge Malindi Zanzibar wa Chama cha Wananchi (CUF), Ally Saleh amesema anataka kukutana na Rais wa Fifa, Gianni Infantino ili kumueleza namna soka la Zanzibar limekuwa likibanwa na Shirikisho la Soka Tanzania Bara (TFF).

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana Saleh alisema TFF imekuwa ikiangalia soka la Bara na kutoangalia soka la visiwani lenye programu nzuri za vijana.

"Zanzibar tuna programu nzuri za vijana, hata kufanya vizuri kwa timu yetu ya Taifa ni vijana ambao wamekuwa wanafanya vizuri katika ligi za vijana zinazoendelea," alisema.

Saleh aliongeza, TFF wamekuwa hawatetei kurejeshwa kwa uanachama wa Zanzibar, baada ya kufutwa uanachama licha ya kwamba awali shikilisho hilo ndio walisaidia kupatikana kwa uanachama awali wa CAF.

"Tumefutiwa uanachama, lakini wenzetu wamefumbia macho, tunataka tuandike barua ya wazi kwa rais wa Fifa ili wajue kama Wazanzibar hatujakubaliana nalo," alisema kiongozi huyo.

Ujumbe wa Fifa umeanza kuingia nchini leo tayari kwa mkutano wao wa kupanga ajenda za mkutano mkuu utakaofanyika Russia wakati wa Kombe la Dunia.

Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidau amezitaja ajenda kuu tatu za mkutano wa Fifa utakaofanyika Dar es Salaam ni kuhusu soka la vijana, kufuata mpangilio ya Fifa, pamoja na changamoto za klabu hasa katika upande wa leseni.

Mapema jana Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe alisema mkutano huo utakuwa na watu sabini na wajumbe wataanza kuwasili nchini kesho (leo), huku rais wa Fifa atawasili siku moja kabla ya mkutano.

"Tunategemea kupokea watu takribani sabini katika kikao hicho, kuanzia kesho ndio wajumbe wataanza kuingia nchini, nitamchukua rais wa fifa na kumpeleka ikulu kuzungumza na rais John Magufuli kisha ndio ataenda katika kikao hicho ambacho hata mimi siruhusiwi kuingia," alisema Mwakyembe.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad