Meli ya uvuvi kutoka Malaysia imekamatwa mjini hapa baada ya kukutwa na mapezi ya samaki aina ya papa na kutozwa faini ya Sh770 milioni.
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina alisema jana kwamba meli hiyo inayomilikiwa na kampuni ya Buah Naga ilikamatwa Januari 26.
Alisema samaki hao ambao wamekatwa hawakuwa na miili yake kinyume cha kanuni ya 66 ya Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu, pamoja na kifungu cha 18 (2) cha Sheria ya Mamlaka ya Uvuvi wa Bahari Kuu ya mwaka 1998 na marekebisho yake ya mwaka 2007.
“Serikali hii mtakaguliwa na kupekuliwa kuliko wakati wowote hivyo ni vizuri mkatii sheria za nchi kwa mujibu wa leseni zenu,: alisema huku kapteni wa meli hiyo, Han Ming Chuan raia wa Taiwan akimsikiliza.
Mpina alisema meli zimekuwa zikitumika pia kufadhili biashara nyingine haramu ikiwamo, usafirishaji haramu wa binadamu, dawa za kulevya na silaha na pia kutorosha nyara za Serikali.
Alisema kitendo cha wamiliki wa meli hiyo kuwakata samaki hao mapezi na kisha kutupa miili yao baharini kimeleta athari kubwa kwa taifa kwani samaki hao wangeweza kutumika kwa matumizi mengine ya binadamu na kuchochea uchumi wa nchi.
Mbali ya faini hiyo, Mpina aliagiza samaki wasioruhusiwa wataifishwe na kugawiwa kwa wananchi wa maeneo jirani ya Manispaa ya Mtwara na kuonya kuwa siku nyingine Serikali ikikamata meli iliyofanya makosa ya aina hiyo itataifishwa kwa mujibu wa sheria.
Kamishna wa Oparesheni wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Luteni Kanali Frederick Milanzi alisema meli hiyo baada ya kukaguliwa imekutwa na kilo 90 za mapezi hayo na bastola yenye risasi 10 ambayo inaendelea kushikiliwa katika ofisi ya mkuu wa upelelezi wa makosa ya jinai Mkoa wa Mtwara hadi hati za umiliki zitakapowasilishwa.
Kaimu Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bahari Kuu, Hosea Mbilinyi alisema hatua zinazochukuliwa zimelenga kudhibiti uvuvi haramu na utoroshaji wa samaki na mazao yake nje ya nchi na kwamba ni endelevu.
Wakili wa Serikali, Wankyo Simon alisema makosa hayo adhabu yake ni kubwa na kwamba wanapaswa kulipa faini hiyo vinginevyo hatua kali zaidi zitachukuliwa dhidi yao ikiwa na pamoja na kapteni kufikishwa Mahakamani.