Mgombea wa Ubunge Kupitia CCM Maulid Mtuli Aahidi Kuibadilisha Tandale

Mgombea wa Ubunge Kupitia CCM Maulid Mtuli Aahidi Kuibadilisha Tandale
Mgombea ubunge Jimbo la Kinondoni kupitia CCM, Maulid Mtulia amesema kwa muda wa miaka miwili alioliongoza jimbo hilo kwa tiketi ya CUF alikuwa mbunge wa mashaka.

Mgombea huyo aliyasema hayo akiwa Kata ya Ndugumbi akiongozwa na Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe na Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson.

Alidai kipindi hiki akichaguliwa atahakikisha barabara ya Argentina na Tandale inajengwa kwa kiwango cha lami huku pembeni zikiwaka taa.

‘’Sikuweza kufanya lolote kwa wakazi wa Ndugumbi wakati nikiwa CUF, lakini sasa mkinichagua najua nitafanya nini,’’ alisema.

“Kwa kuwa nipo kwenye chama dume kilichopewa ridhaa na Watanzania kuleta maendeleo, baada ya kupata ubunge nitakwenda kujenga Mto Mwangosi.’’

Aliongeza kuwa, “Nakwenda kuhakikisha tunatumia pesa za Manispaa ya Kinondoni fungu la vijana, tutawapa mikopo wanunue pikipiki waweze kujiajiri.”

Kwa upande wake, mgombea ubunge Jimbo la Siha kwa tiketi ya CCM, Dk Godwin Mollel aliwaomba wananchi wamrudishe bungeni ili aweze kushirikiana na Serikali kufufua zao la kahawa.

Mgombea huyo pia alisema ataboresha miundombinu ya madarasa ya shule na mazingira ya upatikanaji wa elimu ili kuhakikisha elimu inayotolewa inakuwa bora na si bora elimu.

Akiwa katika Kijiji cha Kengia, Kata ya Kashashi, Dk Mollel alisema uboreshaji wa kahawa utasaidia kuwakomboa wananchi kiuchumi na kuachana na umaskini.

“Sikutumwa bungeni kuandamana na kufunga mdomo, bali kuwasemea na kuwaletea maendeleo. Sasa nitumeni nikakomeshe umaskini Kashashi kwa kufufua zao la kahawa na kuboresha mazingira ya upatikanaji wa elimu,” alisema.

Aliongeza kuwa Kata ya Kashashi inahitaji kusambaziwa umeme, hivyo akichaguliwa atahakikisha wananchi wanafikishiwa nishati hiyo na kuitumia kuanzishia miradi ya maendeleo ili wajikwamue kiuchumi.

Mgombea ubunge kwa tiketi ya CUF Jimbo la Siha, Tumsifueli Mwanri alisema akichaguliwa atahakikisha viwanja vya michezo vinakuwapo kila kijiji na vilivyovamiwa vinarudishwa.

Akizungumza na wananchi wa Kata ya Nasai wakati wa kuomba kura, alisema atahakikisha kila kijiji na kitongoji kunakuwa na viwanja vya michezo.

“Nataka kufufua michezo kwani michezo ni ajira na pia michezo inaboresha afya na kuepusha magonjwa ikiwamo kisukari, nipeni nafasi nifanye kazi,” alisema.

Kwa upande wake, mgombea ubunge wa CUF Jimbo la Kinondoni, Rajabu Salum akiwa Msisiri, Kata ya Makumbusho alisema wanacheleweshewa hati ya viapo vya mawakala wa chama chao.

“Wanataka kutoa hati za viapo siku hiyo ya kupiga kura ili baadaye waonekane wamechelewa nisichaguliwe,” alisema.

Mkutano wa kampeni wa Chadema uliokuwa ufanyike jana stendi ya zamani ya daladala iliyopo Mwenge ulizuiwa kwa kile ambacho Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Aaron Kagurumjuli alisema hawakuwa na ratiba ya kukutana eneo hilo.

Awali, wananchi waliokuwa katika eneo la Mwenge walisema kabla ya mkutano huo kuvunjwa kulikuwa na makada wa CCM waliowahi na kuanzisha mkutano wao.

Hata hivyo, msafara wa mgombea ubunge wa Chadema, Salum Mwalimu ulifika eneo hilo majira ya saa 10 na kukuta mkutano wa CCM ukiendelea, ndipo walipowaonyesha ratiba maofisa wa polisi ambao waliuvunja mkutano huo.

Licha ya kuuvunja mkutano huo wa CCM baadhi ya mashuhuda waliokuwa katika eneo hilo walisema polisi haohao waliwakataza makada wa Chadema akiwemo Mwalimu kuendelea na mkutano jambo lililozua malumbano.

Akizungumza kwa njia ya simu, Kagurumjuli alisema mkutano huo ulivunjwa kwa sababu Chadema hawakuwa na ratiba katika eneo hilo.

“Kwenye ratiba yetu hakukuwa na chama chochote kilichotakiwa kufanya kampeni eneo la Mwenge. Chadema walitakiwa kufanya mkutano eneo la Ali Maua, Kata ya Kijitonyama. Ni makosa kubadilisha eneo la kampeni na ili ubadilishe ni lazima uandike barua,” alisema Kagurumjuli.

“Siyo Chadema tu, hata CCM walikuwa pale baada ya kuona nafasi, lakini tuliwafukuza.”

Hata hivyo, mgombea ubunge wa Chadema, Mwalimu alisema hakukuwa na sababu ya msingi kwa wao kuondolewa eneo la Mwenge kwa kuwa ratiba ilionyesha watakuwa Kata ya Kijitonyama, hivyo wana haki ya kufanya mkutano popote.

“Hakukuwa na sababu yoyote ya kutuondoa pale, hata OCD aliyekuwa pale nilimuuliza akasema hakuna sababu, basi tu kwa sababu ana risasi na mabomu anafanya ubabe,” alilalamika Mwalimu.

“Tulishakubaliana tangu mwanzo kwamba kama chama kimepangiwa kata fulani kinatawala kata yote bila kuingiliwa na chama kingine. Mbona nimefanya kampeni za nyumba kwa nyumba kata yote sijakatazwa?”

“Jeshi la Polisi limedhihirisha wanachotaka kukifanya Februari 17 na sisi hatutakubali kuwa wanyonge maana wanaona kuna wanaume na wavulana. Juzi kiongozi wetu ametekwa na kuuawa, mara wamevamia ofisi yetu na kupiga mabomu, leo wamekataza mkutano wetu. Sisi hatutakubali, tutapambana nao hadi mwisho.”

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi wa Kinondoni, Jumanne Muliro alipoulizwa kwa njia ya simu alisema hana taarifa za kuzuiliwa kwa mkutano huo.

Flora Temba, Bahati Chume (Moshi), Elizaberth Edward, Pamela Chilongola, Fortune Francis, Asna Kaniki, Elias Msuya na Ephrahim Bahem (Dar)
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad