Mkandarasi Mwanza Matatani Waziri Mkuu Atuma TAKUKURU Kumkamata


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amemuagiza kamanda wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) mkoani Mwanza, mhandisi Ernest Makale kumkamata mkandarasi wa kampuni ya Palimon baada ya kushindwa kukamilisha mradi wa maji wa Sh2.06 bilioni.

Taarifa kutoka ofisi ya waziri mkuu imesema kuwa Majaliwa amechukua uamuzi huo leo Februari 16, 2018 wakati akizungumza na watumishi na wananchi kwenye kijiji cha Igumangobo wilayani Kwimba.

Inaeleza kuwa mkandarasi huyo alianza ujenzi wa mradi huo Oktoba 28, 2013 na alitakiwa kukamilisha Mei 28, 2014.

Majaliwa amesema kitendo cha mkandarasi kutokamilisha mradi huo kwa wakati licha ya kupewa fedha hakivumiliki, hivyo ameitaka Takukuru kutafuta popote alipo na kumhoji.

Ametoa agizo hilo baada ya wananchi wa vijiji vya Mhande, Shirima na Izizimba ‘B’ ambao mradi huo unatekelezwa katika vijiji vyao kumuomba waziri mkuu awasaidie ili mradi wao ukamilike na wao wapate huduma ya maji.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amelitaka Baraza la Madiwani la Halmashauri ya wilaya ya Kwimba kutotumia fedha za miradi ya maendeleo kulipana posho.

“Fedha zinazopelekwa si za kulipana posho ni za maboresho na Serikali inataka wananchi wahudumiwe wasipate shida,” amesema.

Awali, Majaliwa alifungua mradi wa maji wa kijiji cha Igumangobo kilichopo Tarafa ya Mwamashimba wilayani Kwimba. Chanzo cha maji hayo ni Ziwa Victoria.

MWANANCHI
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad