Mke wa Tambwe Hiza Aeleza Mazingira ya Dk. za Mwisho za Uhai Wake

Mke wa Tambwe Hiza Aeleza Mazingira ya Dk. za Mwisho za Uhai Wake
WAKATI familia ikikaa na kujipanga jana kwa ajili ya mazishi ya kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tambwe Hiza, mkewe Mariam Masoud, ameelezea mazingira ya dakika za mwisho za uhai wake.


Akizungumza na Nipashe jana, mjane huyo alisema  mume wake hakubahatika hata kufika hospitali kupata matibabu ya kuokoa maisha yake baada ya kubanwa na pumu alfajiri ya jana.

Mariam alisema mumewe alibanwa na ugonjwa huo saa 11:00 alfajiri na ndipo alipowasha gari ili akimbie hospitali kuwahi matibabu.

Alisema, lakini alipotoka tu kwenye uzio wa nyumba yake, alishindwa kuendesha gari na kulisimamisha katikati ya barabara.

Alisema baada ya kuziba barabara, gari la wanafunzi lililokuwa nyuma yake lilimpigia honi muda mrefu kujaribu kumtaka apishe njia, lakini wakati huo alishaishiwa nguvu na hakuwa na uwezo wa kuliendesha.

“Mume wangu huwa anasumbuliwa na pumu pamoja na shinikizo la damu, kwa pamoja kwa muda mrefu sana, na imekuwa ikimbana mara kwa mara na kuna kipindi huwa inazidi, lakini akitumia dawa huwa anapona,” alisema Mariam na kueleza zaidi:

“Na hata humu ndani dawa zake anazotumia huwa zipo wakati wote ikiwamo zile za kupuliza na inapozidi sana huwa anakimbilia hospitali.

“Lakini leo (jana) alfajiri ilimbana tena, kwa hiyo akawa amechukua gari lake na kuendesha mwenyewe ili aende hapo hospitali ya Kizuiani, lakini alifanikiwa kutoka tu hapo nje ya uzio, akashindwa kuendelea na kwa sababu ni barabarani akawa ameziba (njia).

“Dereva wa gari la wanafunzi alipofika na kuona barabara imezibwa akampigia honi na alivyoona hasogei akaenda kumwangalia.

“Alivyomsogelea na kuzungumza naye alimwomba dereva huyo wa wanafunzi amwendeshe hadi hospitali,  lakini kabla ya kufika mbali akawa amekufa humo humo kwenye gari.”

Mariam alisema juzi mume wake alikuwa na nguvu na alikuwa akiendelea vizuri na shughuli zake, ikiwamo kampeni za uchaguzi mdogo Jimbo la Kinondoni.

Kwa upande wake, kaka wa marehemu, Charles Hiza, alisema ni kweli mdogo wake alifariki kwenye gari kabla ya kufika hospitali.

“Hospitali siyo mbali, lakini alifia njiani wakati anapelekwa na huyo dereva wa gari la wanafunzi na alimsaidia baada ya kuona ameshindwa kuendesha gari na akiwa ameziba barabara,” alisema Charles.“Hospitali waliamua tu kupokea maiti na kuthibitisha kuwa amefariki.”

Alisema mwili wa marehemu Tambwe umehifadhiwa katika Hospitali ya Temeke wakati wakisubiri taratibu za mazishi kukamilika.

MIAKA 30Mtoto wa marehemu, Turo Hiza alisema baba yake alikuwa akisumbuliwa na pumu kwa karibu miaka 30 na tatizo hilo limekuwa likimtokea mara kwa mara.

“Kutembea na dawa imekuwa ni kawaida yake... vidonge, sindano (na) hata ya ‘kuspray’ (kupuliza), lakini kwa jana alizidiwa sana kwa sababu pia hakukuwa na mtu wa kumsaidia kuendesha gari,” alisema Turo.

“Kifo cha baba ni pigo kwetu sisi watoto wake, lakini pia ni pigo kwa familia nzima kwa sababu yeye ndiye alikuwa anategemewa sana na kama mnavyojua baba yetu, kama ambavyo alikuwa mcheshi huko kwenye mambo ya kisiasa, ndivyo hivyo alivyokuwa katika familia yake,” alisema mtoto huyo.

“Alikuwa ni rafiki yetu wa karibu, mshauri mkubwa na aliyetegemewa na kila mtu.”

Akizungumza wakati akihojiwa na kituo cha Redio cha East Africa, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu ambaye ni mgombea ubunge Jimbo la Kinondoni, alisema pamoja na kwamba kifo cha Tambwe ni pigo kubwa kwa familia na chama, kwake ni zaidi.

“Kifo cha Tambwe kwangu ni pigo kubwa zaidi, nimemfahamu siku nyingi na ni rafiki yangu mkubwa sana, amekuwa miongoni mwa timu ya kampeni zangu, tumekuwa tukizunguka naye kila siku, kila mahali na amekuwa akiteka hisia za wananchi katika kampeni  kutokana na lugha yake ya ushawishi,” alisema.

“Tambwe hakutakiwa kuniacha katika kipindi hiki, kwa kweli kifo chake kimenishtua sana. Jana (juzi) tulifanya wote kampeni na tulipomaliza kama kawaida, wanachama walitusindikiza mpaka ofisi za Chadema Kanda ya Pwani kwa ajili ya kwenda kufanya tathmini na tulikaa pale hadi majira ya saa tano usiku ndipo tukatawanyika.”

Katibu wa Chadema mkoa wa Dar es Salaam, Henry Kileo, alisema juzi baada ya kampeni za kumnadi Mwalimu, Tambwe alimuuliza maswali mengi ambayo hakuwahi kumuuliza ikiwamo kutaka kupafahamu nyumbani kwake.

“Siku zote tulikuwa naye, lakini juzi aliniuliza maswali ambayo hajawahi kuniuliza,” alisema Kileo.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad