Mkurugenzi Afafanua Mawakala Kuzuiwa Kuingia


Wakati baadhi ya vituo vya kupigia kura katika uchaguzi wa jimbo la Kinondoni mawakala wa vyama vya siasa wamezuiwa kuingia kwa madai kuwa barua zao za viapo zimekosewa, msimamizi wa uchaguzi huo, Aron Kagurumjuli amesema uchaguzi huo unakwenda vizuri.

Baadhi ya mawakala hao katika kituo cha Lasko kilichopo kata ya Tandale wamezuiwa kwa madai kuwa hati zao za uthibitisho walizopewa zimekosewa.

Akizungumza leo Februari 17, 2018 msimamizi wa mawakala wa CUF kata ya Tandale, Abdul Zain amesema wamefika vituoni tangu saa 12 asubuhi lakini mawakala wao wamezuiwa kuingia ndani ya vituo hadi hati zao zitakapobadilishwa.

Amesema kuwa wamefuatilia suala hilo ofisi za Kagurumjuli na kupewa fomu nyingine ambazo pia zimekataliwa.

Katika ufafanuzi wake, Kagurumjuli amesema mawakala wengi hawakuwa na barua kutoka NEC zinazowatambulisha kuwa ni mawakala ambazo walitakiwa kupewa na viongozi wa vyama vyao na badala yake wanatumia barua za viapo alizodai kisheria haziwezi kuwa utambulisho pekee wa kuwa mawakala.

Amefafanua kuwa barua hizo za viapo hazitumiki kuwahalalisha, kwamba vituo vyote katika kata tano wameshatatua tatizo hilo.

“Wakala anapaswa kuapa kwanza na barua ya kiapo napaswa kuwa nayo mimi ili wakifanya kosa niwachukulie hatua. Kiapo si mali yao ndiyo maana tuliwapa nakala, hakuna sheria ya kupewa barua ya kiapo kuna sheria inayosema wakala ataapa siku saba kabla ya uchaguzi na ndivyo ilivyofanyika,” amesema.

“Barua ya utambulisho ndiyo kitu muhimu wanapaswa kuwa nazo ambazo zimetolewa na ofisi ya Mkurugenzi. Barua ya kiapo siyo suluhisho la kuingia nayo kwenye kituo ila barua ya utambulisho ndiyo inahusika.”

Kuhusu matokeo kutangazwa amesema, “Tunatarajia  hadi saa sita usiku matokeo yatakuwa yameshajulikana iwapo kura zitapigwa vizuri na kuhesabiwa bila vurugu.”

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad