Mnyeti Alivunja Baraza la Ardhi

Mnyeti Alivunja Baraza la Ardhi
Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti amelivunja baraza la ardhi la Kata ya Murray wilayani Mbulu mkoani Manyara  baada ya wananchi kulalamika kunyanyaswa, kuombwa rushwa na kunyimwa haki zao.

Akizungumza jana Februari 12, 2018 baada ya kulivunja baraza hilo, Mnyeti amesema hawezi kuliacha liendelee kufanya kazi kwenye eneo hilo wakati wananchi wanalalamikia kukosa haki zao.

Amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya mji wa Mbulu, Anna Mbogo kuanza mchakato wa kupatikana viongozi wapya, waadilifu wa baraza la kata hiyo ili waendelee kuwatumikia wananchi.

Amesema mikutano ya wananchi kuwachagua wajumbe wengine inatakiwa kuanza upya ili nafasi za wajumbe wapya zipatikane na kuhudumia jamii ya eneo hilo.

"Tafuteni watu waadilifu, wenye weledi na hofu ya Mungu ambao wanaweza kuwahudumia wananchi ili washike nafasi hizo na kutekeleza majukumu yao ipasavyo," amesema Mnyeti.

Amesema kuwa baada ya kuwaondoa viongozi wa baraza hilo linalodaiwa kupokea rushwa wananchi waendeshe zoezi la kupatikana majina mapya kisha yapelekwe kwenye vyombo vya uchunguzi.

Mkazi wa kata ya Murray,  Michael Amme amelalamikia baraza hilo akidai kuwa halitendi haki na kuwaonea wananchi wanyonge.

Amme amesema kwa muda mrefu walikuwa wanalalamikia uamuzi wenye harufu ya rushwa kwa maelezo kuwa familia yao iliporwa eneo kutokana na maamuzi mabovu ya baraza hilo.

Hata hivyo, mjumbe wa baraza hilo Verani Anthony amesema wananchi wa eneo hilo wanapaswa kupatiwa elimu juu ya utendaji kazi wao.

Amesema wananchi hao wangepatiwa semina juu ya baraza hilo wasingelalamika kwani wao hutekeleza wajibu wao ipasavyo.

Pia, Mnyeti amemuagiza mkuu wa polisi wilaya ya Mbulu, kumkamata Mwenyekiti wa kijiji cha Murray, John Amme kwa kuwanyanyasa wananchi yakiwamo madai ya kuwapiga.

"OCD mkamate huyo mwenyekiti wa kijiji hiki ili akaeleze huko polisi kwa nini amemvunja mkono mwananchi kwa sababu kupiga watu si wajibu wake," alisema Mnyeti.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad