Simanzi ilitawala jana katika mitandao ya kijamii Afrika Mashariki baada ya kuenea kwa taarifa ya kifo cha mwanamuziki wa Uganda, Moses Sekibooga maarufu Mowzey Radio aliyefariki dunia baada ya kuugua kwa takribani wiki mbili.
Radio aliyewahi kutamba na kundi la Goodlyfe alilazwa katika Hospitali ya Case baada ya kushambuliwa katika ugomvi uliotokea wiki mbili zilizopita katika baa ya De.
Ugomvi huo ulimsababishia apasuke fuvu na kulazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi.
Wasanii mbalimbali nchi za Afrika Mashariki, wamemlilia msanii huyo akiwamo Lady Jay Dee, Profesa Jay, Diamond Platnumz, Vannesa Mdee, Nameless, MwanaFA, Jose Chameleone na Juacali.
Rais wa Uganda, Yowere Museven ni miongoni mwa watu waliotumia mtandao wa Twitter kueleza namna alivyoguswa na msiba wa mwanamuziki akisema nchi hiyo imepoteza nguvu kazi.
Wiki iliyopita Rais Museven alitoa Sh30 milioni za Uganda ili kugharamia matibabu ya mwanamuziki huyo aliyeshiriki katika Kampeni za Urais mwaka 2015.
Mashabiki wafurika hospitali
Polisi walilazimika kuimarisha ulinzi nje ya Hospitali ya Case alipofia mwanamuziki huyo baada ya mashabiki kufurika kila mmoja akitaka kuushuhudia mwili wake.
Ndugu na wanamuziki wengine walifika katika eneo hilo kila mmoja akijaribu kupata nafasi ya kushuhudia mwili wa Radio.
Vilio vililipuka katika eneo hilo baada ya mwanamuziki Weasel aliyekuwa kundi moja na Radio aliyezaliwa Januari 1, 1985, kufika hospitalini hapo. Mashabiki walisikika wakimuuliza kwa simanzi: “Itakuwa vipi Weasel bila Mowzey (Radio)”?
Radio akiwa na Weasel katika kundi la Goodlyfe waliwahi kutamba na nyimbo kama Nakudata, Bread and Butter, Magnetic, Nyambura na Home to Africa.
Wiki iliyopita polisi walimkamata mmiliki wa baa hiyo, George Egesa na rafiki yake Xavier Rukere ili waisaidie polisi kumpata mtuhumiwa anayedaiwa kumpiga mwanamuziki huyo.