Kauli hiyo ya Mzee Akilimali imekuja baada ya Simba kutinga raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho Afrika ambapo sasa itacheza na Al Masry ya Misri Machi 6, mwaka huu.
Akizungumza na Championi Jumamosi, Mzee Akilimali alisema haoni dalili za Simba kufanikiwa kwenda hatua kubwa kufuatia kukutana na Waarabu ambao ni moto wa kuotea mbali katika michuano hiyo.
“Safari hii naona nao wamepata chuma kwa sababu miaka ya nyuma walikuwa wanatucheka kwamba hatuwezi kucheza na Waarabu nao ndiyo walikuwa wanajifanya wanawamudu kwa kuangalia historia.
“Lakini jambo zuri wamepata bahati na wamerejea kwenye michuano ya kimataifa ila sasa wale wanaokutana nao ni chuma cha moto, Simba hawawezi kwenda popote,” alisema Mzee Akilimali.
Al Masry ni miongoni mwa timu ambazo zinatoa upinzani mkali kwa vigogo wa soka Misri ambapo ni Zamalek na Al Ahly na sasa wapo nafasi ya nne katika Ligi ya Misri wakiwa na pointi 42.
Kocha wa Al Masry ni mshambuliaji wa zamani wa Zamalek, Hossam Hassan ambaye alikuwepo kwenye kikosi cha Zamalek kilichong’olewa na Simba mwaka 2003 katika Klabu Bingwa Afrika.