KATIBU wa Baraza la Wazee wa Yanga, Mzee Ibrahim Akilimali, amelitaka benchi la ufundi la timu hiyo linaloongozwa na Mzambia, George Lwandamina, kuhakikisha wanatafuta mbadala wa mchezaji atakayekuwa anapiga penalti badala ya Mzambia, Obrey Chirwa.
Mzee Akilimali ameyasema hayo kufuatia mshambuliaji huyo kuwa na mfululizo wa kukosa penalti ambapo juzi Jumamosi alikosa tena wakati Yanga iliposhinda bao 1-0 dhidi ya St Louis katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliopigwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.
Kwa mwaka huu, Chirwa amepiga jumla ya penalti tano ambapo kati ya hizo kakosa nne dhidi ya URA kwenye Kombe la Mapinduzi, Ihefu katika Kombe la FA, Njombe Mji kwenye Ligi Kuu Bara na St Louis. Aliyopata ni dhidi ya Ihefu ambapo kwenye mchezo huo alipiga penalti mbili.
Akizungumza na Championi Jumatatu, Mzee Akilimali alisema kuwa kwa upande wake analitupia lawama benchi la ufundi la timu hiyo kwa kuendelea kumpa penalti mchezaji huyo licha ya kutokuwa na bahati nazo hali inayowafanya kupata wakati mgumu kupata matokeo.
“Kwangu siwezi kumlaumu Chirwa hata kidogo, wa kulaumiwa ni benchi zima la ufundi likiongozwa na Lwandamina kwa sababu sioni haja ya kuendelea kumtumia penalti aendelee kupiga mchezaji huyo maana hana bahati nazo hata kidogo.
“Siku zote amekuwa akikosa penalti katika michezo muhimu na hii ni (mechi) ya tatu kwake lakini bado amekuwa akikosa, sasa kwa nini wasibadilishe na ukiangalia katika mchezo wa jana (juzi) yeye ndiyo ameigharimu timu kwa kiasi kikubwa lakini walimu sijui hawakuliona hilo au vipi,” alisema Mzee Akilimali.