Mbunge wa Jimbo la Iringa Mjini (CHADEMA), Peter Msigwa amefunguka na kudai nchi ya Tanzania imefika mahali pa hovyo kutokana na watawala kuiendesha nchi kwa mtazamo wao na sio kufuata sheria na kanuni zilizopo.
Msigwa ametoa kauli hiyo wakati alipokuwa akimuombea ridhaa mgombea Ubunge Jimbo la Kinondoni Salum Mwalimu ili aweze kupata kura za ndio kwa wananchi hao siku ya kupiga kura ambapo mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Waziri Mkuu mstaafu na Mjumbe wa Kamati Kuu CHADEMA, Mhe. Edward Lowassa , huku akisindikizwa na mameya na Wabunge mbalimbali kutoka UKAWA.
"Watawala wanaendesha nchi kwa 'personality' na badala ya sheria na kanuni. Kwa bahati mbaya sana wale ambao wanategemewa kusema, kukemea pamoja na kuonya wamekaa kimya. Lakini baadhi yetu tumeamua iwe mvua, jua, iwe mabomu ya polisi, vituo vya polisi hata gereza tutazungumza hatutoogopa mtu yeyote", amesema Msigwa.
Pamoja na hayo, Msigwa ameendelea kwa kusema "nchi ya Tanzania imefika mahali ambako kiongozi hawezi kusemwa, Mkuu wa Mkoa hata Spika wa Bunge".
Kwa upande mwingine, Msigwa amewaambia wananchi wa Jimbo la Kinondoni kwamba wakimuona Mbunge anajikomba komba serikalini basi watambue mtu huyo hatambui wajibu wake anaopaswa kuutekeleza au kuufanya.