Ndugu wa wanandoa waliokamatwa China kujadili malezi ya mtoto


Kamishna wa Intelejensia wa Mamlaka ya Kupambana na Dawa za Kulevya, Frederick Kibuta amesema Jumatatu ijayo mamlaka hiyo itakutana na pande mbili za familia ya wanandoa waliokamatwa China wakiwa wamebeba dawa za kulevya aina ya heroin kukamilisha makabidhiano ya mtoto wa watuhumiwa hao.

Wanandoa hao, Baraka Malali na Ashura Mussa walikamatwa Januari 19 wakiwa na mtoto huyo mwenye umri wa miaka miwili na miezi tisa, ambaye alirejeshwa nchini siku tatu zilizopita.

Kibuta alisema mume na mke hao walikamatwa wakiwa wamemeza kete takribani 127 za dawa za kulevya aina ya heroin.

Mwananchi lilipowasiliana na baba mzazi wa Ashura, Hashimu Mussa Mbaruku ambaye ndiye aliyekabidhiwa mtoto huyo baada ya kurejeshwa nchini, alisema ameshamuozesha mwanae na hana chochote cha kuzungumza juu ya yaliyomkuta. “Sitaki kusumbuliwa kuhusu suala hilo kwa sababu sijui chochote.

“Sitaki usumbufu wa aina yoyote, nyinyi ni waandishi wa habari kazi yenu kutafuta habari mimi sina cha kusema na sitaki kabisa mnisumbue,” alisema Mbaruku.

Kabuta pia ameeleza kupata taarifa katika mitandao ya kijamii juu ya kitengo cha dawa za kulevya nchini India (NCB) kumkamata Mtanzania, Brayton Lyimo (31) akiwa na dawa aina ya heroin.

Taarifa hiyo iliripotiwa juzi katika mitandao ya kijamii ya Mwananchi ikilinukuu gazeti la kila siku la India la New Delhi, likisema Lyimo alikamatwa Jumanne wiki hii kwenye Uwanja wa Ndege wa Indira Ghandhi jijini Delhi.

Kuhusu mke na mume hao, Kabuta alisema walikuwa wakisafirisha dawa hizo walizozimeza kutoka Tanzania kwenda nchini humo. “Walikamatiwa Zhejiang... Hatujajua idadi rasmi, lakini inakadiriwa mwanamke alimeza kete 80 na mume alimeza 47,” alisema.

Alisema mpaka sasa wanaendelea kushikiliwa nchini humo na kwamba mtoto wao amerejeshwa nchini juzi.

“Baada ya kukamatwa, ubalozi wa China nchini Tanzania wamemleta mtoto huyo na wakati anafikishwa hapa babu yake upande wa mama alikuja kumpokea,” alisema.

Kuhusu Mtanzania aliyekamatwa India alisema amesikia kupitia vyombo vya habari vya nje, “Lazima tujiridhishe na ubalozi wetu nchini India ndiyo tutakuwa na cha kuzungumza.” Taarifa za gazeti hilo la India zinaeleza kuwa Mtanzania huyo alikamatwa baada ya kushuka uwanjani hapo akiwa na dawa hizo zenye thamani ya Dola 160,000 za Marekani ambazo ni takribani Sh400 milioni, kwamba alikuwa akitokea Mumbai.

“Alihojiwa na maofisa wa kitengo cha dawa za kulevya baada ya kutiliwa shaka ikiwa ni jitihada za kuzuia genge la kimataifa la biashara ya dawa hizo,” imeeleza taarifa hiyo.

Maofisa wa taasisi hiyo walisema Lyimo alikuwa ameshika vifurushi viwili vya heroin vyenye kilo 4.8.

Taarifa ya maofisa hao inaonyesha kwamba, baada ya kushuka Uwanja wa Mumbai, mtuhumiwa huyo alipanda ndege kuelekea New Delhi ambako alikamatwa.

Ilielezwa pia kwamba dawa hizo zilitokea nchini Tanzania na alitakiwa kuziwasilisha kwa raia wa Nigeria aishie New Delhi.

Ilielezwa pia kuwa, Mtanzania huyo alishafanya safari nyingine ya kwenda India Januari mwaka jana.

Mkurugenzi wa kitengo cha dawa za kulevya India, Madho Singh alisema wanaendelea na uchunguzi zaidi, huku wakichunguza mawasiliano aliyofanya sehemu mbalimbali.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad