LICHA ya kuhamasika kusaka ushindi kwa udi na uvumba ili kupunguza wigo wa pointi saba inazozidiwa na watani zao Simba, mabingwa watetezi, Yanga, wameambiwa na wapinzani wao Njombe Mji kuwa wasitarajie mteremko katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam leo.
Katika mchezo wa kwanza uliochezwa mkoani Njombe, mabingwa hao walipata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya wenyeji hao ambao walipanda daraja msimu huu sambamba na Singida United na Lipuli FC.
Akizungumza na gazeti hili jana, Kocha Msaidizi wa Yanga, Shadrack Nsajigwa, alisema kuwa huu ni wakati wa lala salama na kilichoko katika mipango yao ni kushinda kila mchezo.
Nsajisgwa alisema kuwa kama watashinda mechi zao zote zilizosalia ikiwamo dhidi ya vinara Simba na Azam FC, anaamini nafasi ya kutetea ubingwa wanaoushikilia itawezekana.
Beki na nahodha huyo wa zamani wa Yanga inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa, alisema mechi zote za ligi ni ngumu na wamejiandaa kukabiliana na ushindani kutoka kwa timu zote 16 zinazoshiriki ligi hiyo.
"Wachezaji wetu wanafahamu ugumu na ushindani uliopo katika ligi, tunawakumbusha kupambana katika dakika zote 90 kwa sababu tunaamini hakuna mechi nyepesi, kuhusu majeruhi, tunajua tutakavyoipanga timu na kila mchezaji aliyesajiliwa ana uwezo wa kuitumikia Yanga," alisema kocha huyo.
Kwa upande wa Kaimu Kocha Mkuu wa Njombe Mji, Mrage Kabange, alisema jana kuwa wamekuja Dar es Salaam kushindana na kuondoka na pointi.
"Haijalishi tunacheza ugenini, mpira hauna hivyo siku hizi, kikubwa tunaifahamu Yanga na tumejipanga kupambana nao uwanjani na si kuangalia ukubwa wa jina la klabu yao," alisema Kabange.
Baada ya mechi ya leo, Yanga itaendelea na maandalizi ya kuwakabili St Louise kutoka Shelisheli katika mchezo wa raundi ya awali ya mashindano ya Ligi ya Mabingwa Afrika utakaochezwa Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.