Nondo za Azamu Zarejea Mazoezini Tayari kwa Ajiri ya Kuivaa Sigida United

Nondo za Azamu Zarejea Mazoezini Tayari kwa Ajiri ya Kuivaa Sigida United
Wachezaji wawili wa Azam FC, Nahodha Himid Mao ‘Ninja’ na mshambuliaji Wazir Junior, wamerejea rasmi mazoezini jana baada ya kukosekana dimbani kwa muda mrefu wakiuguza majeraha yanayowakabili.

Himid alikuwa akisumbuliwa na maumivu chini ya goti la mguu wake wa kulia huku Junior akikabiliana na tatizo kwenye kifundo chake cha mguu wa kulia, na tayari nyota hao wameanza kupata nafuu na sasa wanamalizia programu ya mazoezi mepesi kabla ya kuruhusiwa kurejea rasmi katika ushindani.

Nyota hao wamerejea wakati kikosi cha Mabingwa hao wa Afrika Mashariki na Kati (CECAFA Kagame Cup) kikijiandaa na mchezo ujao wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) dhidi ya Singida United, utakaofanyika Uwanja wa Azam Complex Jumamosi hii saa 1.00 usiku.

Junior anayetakiwa kufanya programu hiyo ya mazoezi mepesi kwa muda wa wiki moja, alisema anamshukuru Mungu kurejea tena dimbani huku akikiri kuwa ‘amemiss’ kucheza mpira.

Kikubwa ni kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kurudi tena na nitaendelea kujituma kama ilivyokuwa awali kutokana na majeruhi haya ndo ilikuwa hivyo lakini tutapambana kama ilivyokuwa mwanzo, nimeumiss sana mpira nimemiss sana kucheza mpira na kuonyesha vile mashabiki wanataka.

Lakini naamini kwa rehema za mwenyezi Mungu tutakaporejea tena basi mashabiki watafurahia vile walivyokuwa wakivisubiria, alisema Junior

Mchezo huo unatarajia kuwa mkali na wa aina yake kutokana na ushindani wa timu hizo uliokuwa kwa siku za hivi karibuni, tokea Singida United irejee Ligi Kuu msimu huu, ambapo katika mtanange wa mzunguko wa kwanza uliofanyika Uwanja wa Jamhuri, Dodoma, timu hizo zilitoka sare ya bao 1-1.

Mbali na kukutana katika ligi, pia mwanzoni mwa mwaka huu zilikipiga kwenye nusu fainali ya Kombe la Mapinduzi, ambalo Azam FC imelitwaa, licha ya matajiri hao wa viunga vya Azam Complex kukutana na upinzani mkali, walifanikiwa kushinda bao 1-0, lililowekwa kimiani kiufundi na Shaaban Idd.

Ushindi wa Azam FC kwenye mchezo huo utaifanya kuzifukuzia timu mbili za juu, Yanga iliyo na mchezo mmoja mkononi ikiwa nafasi ya pili kwa pointi 37 na Simba ambayo ipo kileleni kwa pointi 45, pia itaipa nafasi ya kuongeza pengo la pointi dhidi ya timu hiyo kutoka Singida, kwa sasa zikipishana pointi moja kwenye nafasi ya tatu na nne, Azam FC ikiwa nazo 35 na Singida 34.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad