MPIMA Ardhi wa Halmashauri ya Mji wa Kahama, Thobias Patrick, jana alimwaga machozi mbele ya Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi, wakati akijitetea kuhusu tuhuma za kupima eneo la serikali na kujimilikisha kisha kuliuza.
Patrick alikumbana na kadhia hiyo wakati wa ziara ya Waziri Lukuvi katika kampeni yake ya ‘Funguka kwa Waziri’ baada ya wakazi wa mji huo kumfikishia Waziri tuhuma zinazomkabili ofisa huyo.
Baada ya kupata tuhuma hizo, Lukuvi alitembelea eneo hilo na kumhoji ofisa huyo kwa nini alipima eneo la serikali na kumilikisha watu binafsi na yeye akiwa mmiliki wa kiwanja kimojawapo na kisha kukiuza.
Kutokana na swali hilo, Patrick alipata wakati mgumu kujibu tuhuma hizo ambazo zimekuwa zikimkabili kwa muda mrefu, hivyo kujikuta akitokwa machozi huku akijitetea kuwa eneo linalohusishwa na tuhuma hizo si lake kwa kuwa yeye aliuza kiwanja namba 590 Block N na si hicho anachotuhumiwa kukiuza.
Waziri Lukuvi alimwonya ofisa huyo kutojihusisha na ununuzi wa maeneo yenye utata wakati akijua yeye ni mtumishi wa serikali tena akiwa ofisa anayehusika na upimaji wa maeneo hayo.
Waziri Lukuvi yuko katika ziara zake za kukutana na wananchi walio na migogoro ya ardhi na kuitatua ana kwa ana.
Kwa sasa anaendelea na ziara yake kutatua migogoro ya ardhi katika kampeni yake ya ‘Funguka kwa Waziri’.
Hadi sasa ameshasikiliza na kutatua zaidi ya kero na migogoro 2,000 katika mkoa wa Dar es Salaam na wilaya zake za Ilala, Kinondoni na Temeke, mkoa wa Kagera katika Wilaya za Karagwe, Kyerwa na Ngara na kwa upande wa Shinyanga wilaya ya Kahama.
Baada ya Shinyanga, Lukuvi anataraji kufanya ziara katika mkoa wa Pwani ambako kuna migogoro mingi ya ardhi ya muda mrefu kabla ya kwenda maeneo mengine Tanzania Bara.