Wanachama 11 wa Chadema, akiwamo Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kasange, Wilaya ya Ngara mkoani Kagera, Zedekia Yusuf wamejivua uanachama na kutimkia Chama cha Mapinduzi (CCM).
Akiwaongoza wenzake kutangaza uamuzi huo wakati wa sherehe za maadhimisho ya miaka 41 ya kuzaliwa kwa CCM zilizofanyika kiwilaya katika Kijiji cha Kasange, Yusuf ametaja migogoro baina yake viongozi na wenzake wa Chadema kuwa miongoni mwa sababu za yeye kutimkia CCM.
Ametaja sababu nyingine kuwa ni viongozi wenzake kukwamisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwamo ujenzi wa miundombinu ya barabara, miradi ya elimu, afya na maji.
“Kwa bahati mbaya, wajumbe 13 kati ya 25 wa Serikali ya kijiji ambao wanatokana na Chadema ndiyo walikuwa kikwazo kwa kupitisha uamuzi, baadhi wanaonekana kuwa wachochezi ikiwamo kugomea michango ya miradi ya maendeleo,” amesema Yusuf.
Akipokea wanachama hao wapya, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM mkoani Kagera, Issa Samma amewataka kushirikiana na wenzao waliowakuta ili kukijenga chama tayari kwa ajili ya ushindi katika chaguzi mbalimbali zijazo.
Akizungumzia wanachama wa chama chake kuhamia CCM, Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Ngara, Kennedy Stafford amesema licha ya kuonyesha kutojali hisia na imani ya wananchi waliowachagua, mwenyekiti huyo na wenzake wana haki ya kikatiba na kisheria kujiunga na chama chochote cha siasa wanachokipenda.