Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni ACP Jumanne Murilo amekanusha habari za polisi kuvamia ofisi za CHADEMA zilizopo maeneo ya magomeni na kusema kuwa wao walirusha mabomu ili kutawanya watu waliokuwa wakiandamana kwa mwamvuli wa vyama vya siasa.
Kamanda Murilo ametoa kauli hiyo leo wakati akifanya mahojiano kwa njia ya simu katika kipindi cha East Africa Breakfast na kusema kwamba walichokifanya jana jeshi la polisi ni kuzuia vitendo ambavyo vinaweza kuvunja sheria kwa kutumia muamvuli wa vyama vya siasa.
Akizidi kufafanua Kamanda Murilo amesema kwamba suala la ofisi za CHADEMA kuvamiwa yeye analisikia tu mitaani kwani anachofahamu askari walikuwa wakitawanya vijana zaidi ya 100 waliokuwa barabarani kwa mtindo wa maandamano yasiyo na kibali.
"Sisi hatujavamia. Suala la kuvamia nalisiakia tu mitaani. Sisi tunafanya kazi kwa kujitambua na kufanya kazi kwa misingi ya sheria. Mikutano ilianza vizuri na kuisha cha ajabu kilijitokeza kikundi cha watu zaidi ya 100 barabarani na kuanza maandamano ambayo yanasababisha usumbufu kwa watumiaji wengine wa barabara" amesema ACP Murilo.
Ameongeza kuwa "Vijana 100 wakiwa barabaran wanakuwa na mihemuko na wengine wanaweza kutumia mwanya wa kisiasa kufanya uhalifu, Hatuwezi kuacha hizo rapsha zikatokea. Hatutavumilia. Tulipiga mabomu 4 ya machozi kuwatawanya watu waliokuwa wakiandamana".
Pamoja na hayo Kamanda Murilo amesema Polisi wamewashikilia watu waliokuwa wameingia barabarani wapatao kama 15 na kati yao hakuna viongozi kwa kudai kuwa viongozi wamejitahidi kuwa makini.
Akizungumzia kuwepo na kamera za kurekodi matukio kwenye kampeni Murilo amesema ni jukumu lao la kazi la kufuatilia kila linalotokea katika mikutano hiyo huku akisema kutokana na kamera hizo kufanya kazi kwa uwazi kumepunguza hata maneno ambayo yanaweza kuleta shida.