Rais Magufuli Amlilia Kingunge "Ametuachia Somo la Kupigania Maslahi ya Nchi"

Rais Magufuli Apokea kwa Huzuni Kifo cha Kingunge "Ametuachia Somo la Kupigania Maslahi ya Nchi"
February 2, 2018 Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amepokea kwa huzuni na masikitiko taarifa za kifo cha mmoja wa waasisi wa Taifa na mwanasiasa mkongwe nchini Mzee Kingunge Ngombale Mwiru kilichotokea saa 10:30 alfajiri katika Hospitali ya Taifa Muhimbili Jijini Dar es Salaam.

Mzee Kingunge Ngombale Mwiru alikuwa akipatiwa matibabu hospitalini hapo baada ya kushambuliwa na mbwa wake nyumbani kwake December 22, 2017.

Rais Magufuli amesema Taifa limempoteza mtu muhimu ambaye alitoa mchango mkubwa katika juhudi za kupigania uhuru na baada ya kupata uhuru akiwa mtumishi mtiifu wa Chama cha TANU na baadaye Chama Cha Mapinduzi (CCM), na katika nyadhifa mbalimbali za uongozi ndani ya Serikali.

“Mzee Kingunge Ngombale Mwiru ametoa mchango mkubwa sana, sisi kama Taifa hatuwezi kusahau na tutayaenzi mema yote aliyoyafanya wakati wa utumishi wake uliotukuka, ametuachia somo la kupigania maslahi ya nchi wakati wote, kuwa wazalendo wa kweli, kudumisha amani na mshikamano, kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa na kuwa na nidhamu”-Rais Magufuli.

Pia Rais Magufuli amewapa pole wanafamilia wote, wanachama wa CCM, ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na msiba huu, na amewaombea kuwa na moyo wa subira, uvumilivu na ustahimilivu katika kipindi hiki cha majonzi.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad