Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma amesema kwamba hajafanya kosa lolote, hivyo hawezi kujiuzulu kama chama chake cha African National Congress (ANC) kilivyokuwa kikimtaka afanye leo.
Rais Zuma ameyasema hayo alipokuwa akifanya mahojiano na kituo cha runinga cha SABC cha Afrika Kusini, baada ya chama chake kumtaka kujiuzulu kabla ya siku kuisha ama vinginevyo bunge litapiga kura ya kutokuwa na imani naye kesho.
Kumekuwepo na mashinikizo mbalimbali ya kumtaka Rais Zuma ajiuzulu kutokana na tuhuma mbalimbali za rushwa zinazomkabili.
Rais Zuma amesema, chama hicho na wengine wote wanaomtaka ajiuzulu hawamtendei haki kwa sababu hakuna hata mmoja anayetoa sababu au kumwambia ametenda kosa gani hadi kustahili kujiuzulu.
Zuma amesema kwamba hapingani na chama hicho, lakini hakubaliani na uamuzi wanaotaka kuuchukua wa kumshinikiza ajiuzulu. Amesema alikubali kujiuzulu baada ya mwezi Juni, lakini walimkatalia.
Amesema kwamba licha ya mahojiano aliyoyafanya atatoa taarifa zaidi kuhusu shinikizo hilo. Aidha, ANC wamesema kwamba wamesikia kauli ya Rais Zuma na kwamba watatoa taarifa kamili baada ya kupata taarifa rasmi ya kiongozi huyo.
Mapema, kiongozi wa ANC, Jackson Mthembu alisema kuwa, kura ya kutokuwa na imani na Rais itapigwa bungeni Alhamisi ili Rais aondolewe, na Mwenyekiti wa ANC, Cyril Ramaphosa aatapishwa mara moja kuliongoza taifa hilo.
Kamati Kuu ya ANC ilikubaliana siku ya Jumanne kwamba Rais Zuma ajiuzulu ambapo walimtaka kufanya hivyo kabla ya Jumatano kuisha.
Wakati wa mahojiano yake, Rais Zuma hakuzungumzia jambo lolote kuhusu familia ya Guptas, ambayo inadaiwa kutumia ukaribu wake na Rais Zuma, kufanya ushawishi katika masuala mbalimbali ya kisiasa na kiuchumi nchini Afrika Kusini.