Sadifa: Sikuwa na Kosa Ila Namuachia Mungu

Sadifa: Sikuwa na Kosa Ila Namuachia Mungu
Wakati mahakama ikimuachia baada ya Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (Takukuru) kueleza kuwa haina nia ya kuendelea na kesi, aliyekuwa mwenyekiti wa UVCCM, Sadifa Juma Hamis amesema anajua hakuwa na kosa ila anamuachia Mungu.

Sadifa alitoa kauli hiyo jana baada ya kuachiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Dodoma baada ya mashtaka kuwasilisha maombi ya kuifuta kesi hiyo iliyofunguliwa mwaka jana.

Wakili wa Takukuru, Biswaro Biswaro aliwasilisha maombi ya kuifuta kesi hiyo kwa hakimu mkazi mfawidhi wa Mahakama hiyo, Joseph Fovo.

Biswaro alisema kesi hiyo jana ilitakiwa kutajwa lakini wamewasilisha maombi ya kuifuta chini ya kifungu cha 68(a) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai.

Baada ya maelezo hayo, Hakimu Fovo alisema mahakama inakubaliana na maombi hayo na inaondoa kesi hiyo.

Alisema mshtakiwa atakuwa huru kwa sasa na kuwa uamuzi huo hautazuia kukamatwa tena kwa kosa hilo kama upande wa Jamhuri utaona kuna sababu ya kufanya hivyo.

Akizungumza nje ya Mahakama, Sadifa ambaye alikuwa anatetewa na wakili Godfrey Wasonga, alisema: “Uamuzi ya Mahakama kwangu naona ni sahihi na mimi naona sina hatia kwa sababu sina kosa lolote, kubwa zaidi ninaloweza kusema ni kumuachia Mungu.”

Sadifa ambaye pia ni mbunge wa Donge (CCM, alisema binafsi amesoma sheria kwa kiasi kikubwa alijua hakuwa na kosa na kuhoji: “Mtu akija nyumbani kwako kwa utamaduni wa Kitanzania akinywa soda ni kosa?”

Desemba 11 mwaka jana Sadifa alifikishwa mahakamani hapo akituhumiwa na makosa mawili ya utoaji wa rushwa.

Mbunge huyo alidaiwa kutenda makosa hayo Desemba 9 mwaka huu katika makazi yake kata ya Mnada mjini Dodoma akiwa kama Mwenyekiti wa Taifa UVCCM na mwajiri wa umoja huo   
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad