Sakata la Klabu ya Yanga kuzuiliwa kufanya mazoezi katika uwanja wa Taifa lililotokea siku ya jana (Alhamisi) limezua sura mpya na kufanya Waziri mwenye dhamana Dkt. Harrison Mwakyembe kulitolea ufafanuzi Bungeni.
Dkt. Mwakyembe ametoa ufafanuzi huo leo (Ijumaa) katika mkutano wa 10 kikao cha nane cha Bunge kilichomalizika kwa kuhairishwa shughuli zake mpaka Aprili 03, mwaka 2018 mjini Dodoma wakati alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Mchinga (CUF), Hamidu Bobali ambapo aliitaka serikali kupitia Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo iingilie kati suala la timu za Tanzania zikienda kucheza kimataifa huwa zinawekewa zengwe lakini wao wakija kucheza huku wanapewa kipaumbele baadhi ya vitu.
"Haturuhisiwi hicho kiwanja kukitumikisha kubeba michezo zaidi ya mitatu kwa wiki moja na endapo utafanya hivyo unaingiza uswahili na hata kikiharibika huwezi kwenda kudai kwa mtu aliyekupa 'guranty' kwamba kitaka zaidi ya miaka 10", amesema Dkt. Mwakyembe.
Pamoja na hayo, Dkt. Mwakyembe ameendelea kwa kusema "kwa hiyo wiki hii tuna mechi mbili muhimu kesho (Jumamosi) wanacheza Yanga dhidi ya St. Louis na kesho kutwa wanaingia Simba SC (Jumapili) kucheza na timu kutoka Djibout. Kanuni za kimataifa zinataka timu ngeni hiyo ya kimataifa lazima ifanye mazoezi katika kiwanja ambacho kitachezwa mechi hiyo lakini hata FIFA wanatambua hicho kiwanja ni cha timu za hapa nchini. Kwa hiyo Yanga na Simba wanaufahamu vizuri uwanja huo ndio maana wakapewa kipaumbele wageni ili waweze nao kuujua".
Aidha, Dkt. Mwakyembe amesema anahisi kuna uswahili umeshaanza kuingia katika uwanja wa Taifa na kutaka baadhi ya watu kushughulikiwa.
"Uswahili umeshaanza kuingia katika uwanja wetu wa Taifa, na mimi nashukuru kwa haya maneno niliyoyapata nadhani kuna vijana wangu pale wanahitaji wadhibitiwe kwa kweli. Kwa hiyo nataka nifafanue kwamba ni haki ya wageni wapewe nafasi ya kufanya mazoezi na sisi tukafanyie katika viwanja vingine", amesisitiza Dkt. Mwakeymbe.
Kwa upande mwingine, Dkt. Mwakyembe amesema ili uwanja huo uweze kutunzika katika mazingira mazuri bila ya kuharibiwa jambo lolote ndani ya miaka 10 ni lazima yawepo masharti ya utumiaji.