Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amesema baadhi ya wafanyabiashara kutokuwa waaminifu ni moja ya sababu ya Serikali kuzuia vibali vya kuagiza sukari ya viwandani nje ya nchi.
Akizungumza katika ziara ya kikazi ya siku nne iliyoanza jana Februari 9, 2018 baada ya kutembelea kiwanda cha Food and Beverage kilichopo Ipogola ndani ya Manispaa ya Iringa, amesema Serikali ipo katika uhakiki wa viwanda.
Amesema baada ya uhakiki kukamilika wamiliki wa viwanda watapatiwa vibali vya kuagiza Sukari.
"Serikali imekusudia kukuza sekta ya viwanda tunahitaji mageuzi ya kiuchumi na katika utekelezaji wa jambo hilo, ni lazima tuchukue tahadhari kudhibiti mianya yoyote ya uchakachuaji kwa manufaa ya wachache,” amesema.
" Katika suala la sukari kumekuwa na udanganyifu, wapo watu waliagiza sukari kwa madai kuwa ni ya viwanda lakini ilipofika waliisambaza na kuiuza mitaani.”
Katika hatua nyingine, Suluhu amewataka wakazi wa Iringa kutunza amani ili kuwezesha mazingira salama ya uwekezaji na ukuzaji wa uchumi.
"Hivi sasa tunaelekea Tanzania ya viwanda tunajenga uchumi wa viwanda ninaomba mtambue kuwa mahali popote penye vurugu hapawezi kufanyika uwekezaji wala kutengeneza fursa za uchumi,” amesema.
Awali akitoa taarifa ya mkoa, mkuu wa mkoa huo, Amina Masenza amesema hadi kufikia Desemba 2017 mkoa huo ulikuwa na viwanda 695 na kati ya hivyo vikubwa vipo 21 na vya kati 35 na vingine ni viwanda vidogo na vidogo zaidi huku sekta hiyo ikiwa imeajiri watu 15,000 sawa na asimilia 1.6 ya wakazi wa Iringa kwa mjibu wa sensa ya watu na makazi ya 2012.