Serikali inatarajia kutoa chanjo kwa wasichana 614,734 wenye umri wa miaka 14 nchini ili kuwakinga na saratani ya shingo ya kizazi.
Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema hayo leo Februari 27,2018 katika mkutano wa wadau wa chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi.
Mkutano huo umewashirikisha viongozi wa dini na wadau wa sekta ya afya.
Ummy amesema Serikali itaanza kuchanja wasichana wa umri huo ambao hawajaanza vitendo vya kujamiiana waliozaliwa kati ya mwaka 2003 na 2004.
Amesema kutokana na mazingira ya upatikanaji wa chanjo hiyo na gharama kuwa kubwa, wataitoa kwa wasichana wenye miaka 14.
Ummy alisema ilipaswa kutolewa kwa wasichana wa kati ya miaka 9 hadi 14.
“Gharama ni Sh30,000 kwa kila msichana wakati Sh5.5 milioni hutumika kumtibu mgonjwa mmoja wa saratani katika Taasisi ya Ocean Road," amesema Waziri Ummy.