Serikali imeahidi kuwashughulikia Askari Polisi watakao bainika kutesa na kuwapiga raia wakiwa kizuizini, kwa kuwa vitendo hivyo ni kinyume na sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai sura ya 20 kifungu cha 11.
Kauli hiyo imetolewa jana Februari 10, 2018 Bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Eng. Hamad Masauni wakati akijibu swali la Mbunge Viti Maalum Rungwe (Chadema) Sofia Mwakagenda lilohoji kama kuna sheria inayomruhusu Askari Polisi kumkamata mtuhumiwa na kumpiga na kumtesa kabla ya kufikisha kituo cha polisi.
Eng. Masauni alisema serikali kupitia wizara yake imekuwa ikiwachukulia hatua Askari Polisi wanaofanya makosa mbalimbali, ambapo katika kipindi cha mwezi Januari hadi Disemba mwaka 2017, jumla ya askari polisi 105 waliotenda makosa mbalimbali wamechukuliwa hatua za kinidhamu ikiwa pamoja na kufukuzwa kazi.
“Kwa mujibu wa sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai sura 20 kifungu 11 kinaeleza namna ya ukamataji, aidha kifungu hiki mahsusi cha ukamataji hakimruhusu askari kumpiga na kumtesa raia akiwa kizuizuni, kwa mujibu wa kanuni za utendaji wa jeshi la polisi askari yeyote atakayebainika kutesa, kupiga raia akiwa kizuizini huchukuliwa hatua za kinidhamu ikiwemo kufukuzwa kazi au kufikishwa mahakamani,” alisema.