Serikali Yawapa Onyo Wanaojidunga Sindano Kuongeza Maumbile

Serikali Yawapa Onyo Wanaojidunga Sindano Kuongeza Maumbile
SERIKALI imeonya kuwa dawa za kuongeza maumbile zina madhara makubwa katika mwili wa binadamu, ikiwamo kusababisha saratani hivyo kuwaasa wananchi kukubaliana na uumbaji wa Mungu.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto,  Dk. Faustine Ndugulile, alisema hayo jana mjini hapa, alipokuwa akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Suzan Lyimo.

Katika swali lake, Lyimo alihoji athari za kiafya kwa wanaoongeza maumbile kwa kujichoma sindano au kutumia dawa na serikali inatoa tamko gani kuhusu hilo.

"Kumekuwapo na matumizi ya dawa au sindano za kuongeza makalio na matiti, nataka kujua kuna athari yoyote kiafya na kama ndiyo serikali inatoa tamko gani?" alihoji.

Akijibu swali hilo, Dk. Ndugulile alisema sindano, vipodozi na dawa zingine zinazotumika kuongeza maumbile, zina madhara makubwa kwenye mwili ikiwamo kusababisha saratani.

“Mwenyezi Mungu alituumba kila mtu kwa aina yake, kwa rangi yake na maumbile yake. Nyongeza  hizi kitaalam zina madhara kama vilivyo vipodozi haramu.

“Ngozi ina matumizi yake Mwenyezi Mungu hakuiweka pale kwa makosa. Inatusaidia kujikinga na mionzi, kujikinga na magonjwa na matumizi ya vipodozi yanaleta madhara katika ngozi. Pia  yanasababisha mtu kupata saratani,” alisema Dk. Ndugulile.

Aliongeza kuwa: “Kauli yangu kwa wananchi waache kutumia vipodozi hivi na dawa hizi. Mwenyezi Mungu alituumba na makusudio yake tuendelee kwa maumbile na rangi zetu,”.

Katika swali la msingi, Mbunge wa Shaurimoyo, Mattar Ally  Salum (CCM), alihoji serikali ina mpango gani madhubuti wa kuzuia uingizwaji wa vipodozi visivyokuwa na viwango.

"Je, serikali inaweza kutumia fedha kiasi gani kuzuia bidhaa hizo kuingia  nchini? Je, adhabu gani inatolewa kwa yeyote anayekamatwa akiingiza nchini vipodozi visivyofaa kwa matumizi?" alihoji.

Akijibu swali hilo, Dk. Ndugulile alisema Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kudhibiti uingizwaji na utumiaji wa vipodozi hivyo.

Alisema mpaka sasa TFDA imesajili vipodozi 3,179 ambavyo ndivyo vinavyoruhusiwa kuingizwa na kutumika nchini.

Aidha, Dk. Ngugulile alisema  katika mwaka wa fedha wa 2016/17 maeneo 3,648 yalikaguliwa na kati ya hayo,  120 yalikutwa na vipodozi ambavyo havina viwango vinavyofaa kwa matumizi ya binadamu na wahusika walichukuliwa hatua za kisheria.

Pia alisema tani 407.82 za vipodozi vilivyopigwa marufuku vyenye thamani  ya Sh.  bilioni 1.36 ziliteketezwa na TFDA na kesi 52 zilifunguliwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.

Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad