Hayo yamesemwa jana Bungeni Mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndugulile wakati akijibu swali la Mbunge wa Mtambwe, Khalifa Mohammed Issa aliyehoji juu mpango serikali katika kudhibiti biashara ya ngono na madanguro ili kupunguza maambukizi mapya ya Virusi vya Ukimwi (VVU) nchini.
Akijibu swali la Issa, Dkt. Ndugulile alisema Serikali inaandaa mikakati mbalimbali ikiwemo utoaji wa elimu kuhusu madhara ya biashara ya ngono kwa jamii pamoja na kuchukua hatua za kisheria kwa wanaojihusisha na baishara hiyo, pamoja na kudhibiti uwepo wa madanguro.
Katika hatua nyingine, Dkt. Ndugulile alisema serikali inaendelea kuchukua hatua katika kudhibiti mila na desturi potofu zinazochangia maambukizi mapya ya VVU, ikiwemo ukeketaji na urithishaji wa wajane kwa ndugu wa mume, kwa kutoa elimu kwa jamii juu ya madhara ya mila potofu pamoja na kutoa hamasa kwa wakunga wa jadi wanaojihusisha na ukeketaji.