Serikali imetangaza neema kwa watumishi wake wote wanaoidai malimbikizo ya madeni kwa kueleza kuwa itaanza kuyalipa madeni hayo ndani ya mwezi huu wa Februri 2018.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Waziri wa Fedha na Mipango ameeleza kuwa mwisho wa mwezi Februari 2018, serikali itawalipa kwa mkupuo mmoja watumishi wake wote malimbikizo ya madeni na madai yote yaliyoonekana kuwa sahihi.
“Madai yanayostahili kulipwa yanajumuisha shilingi Bilioni 16.25 kwa walimu 15,919, na Tsh. Bilioni 27.15 kwa watumishi 11,470 wasiokuwa walimu. Madai yote yaliyoonekana kuwa sahihi ya TZS Bilioni 43.39 yatalipwa pamoja na mshahara wa mwezi Februari 2018 kwa mkupuo mmoja,” amesema Waziri Mpango.
Ameongeza kuwa kwa malipo ya madai haya ambayo kwa baadhi ya watumishi yana muda wa zaidi ya miaka kumi, majina ya wadai yatatangazwa kwenye magazeti kuanzia kesho Jumamosi februari 10, 2018.
“Malipo ya madai haya ambayo mengine yana zaidi ya miaka 10, majina ya walipwaji yatatangazwa kwenye magazeti kuanzia kesho tarehe 10 Februari, 2018,” amesema Waziri Mpango.
Waziri Mpango amesema madai haya yanajumuisha malimbikizo ya mishahara, nyongeza ya mishahara pamoja na tofauti ya mishahara kutokana na kukaimu nafasi.
“Madai haya yalijumuisha mishahara isiyolipwa, tofauti ya mishahara kutokana na kukaimu na nyongeza za mishahara zilizotokana na kupandishwa vyeo na kuchelewa kurekebishiwa mishahara… Madai ya watumishi 27,389 kati 82,111 yenye jumla ya shilingi Bilioni 43.39 ikiwa ni 34% ya madai yote, yalihakikiwa na kuonekana ni sahihi na yanastahili kulipwa bila marekebisho” amesema.
Aidha amesema kutokana na zoezi la uhakiki lililofanyika, serikali imeweza kuokoa kiasi cha shilingi bilioni 84.22 ambazo ni sawa na 66% ya madai yote zilizokuwa zilipwe kimakosa kutokana na uwepo wa watumishi wengi wenye vyeti feki.
“Zoezi la uhakiki wa madai ya malimbikizo ya mishahara uliofanyika, limeweza kuokoa jumla ya shilingi bilioni 84.22 ambazo ni sawa na 66% ya madai yote ya malimbikizo ya awali ya shilingi bilioni 127.61 yaliyokuwa kwenye mfumo… Kama tungekurupuka tu tukalipa, tungekuwa tumetumia vibaya fedha za watanzania shilingi bilioni 84.22,” amesema Waziri.
Vile vile amesema kuwa serikali itaendelea kulipa madeni yote ya watumishi kadiri yanavyojitokeza ili kuepukana na malimbikizo ambayo kwa namna moja au nyingine, yanaweza kuisababishia serikali hasara.
“Serikali itaendelea kulipa madai ya watumishi kadiri yanavyojitokeza, ili kuondokana na malimbikizo ya aina hii ambayo yanaweza kuisababishia serikali hasara kwa kulipa madai yasiyostahili,” amesema.