Tamisemi Yatolea Ufafanuzi Tamko la RC Makonda

Tamisemi Yatolea Ufafanuzi Tamko la RC Makonda
Tamko la Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda kusimamisha shughuli za mabaraza ya ardhi ya kata limetolewa ufafanuzi, Tamisemi imesema.

Jumamosi iliyopita Makonda akipokea ripoti kutoka kwa wanasheria waliosikiliza kero za wananchi kwa uratibu wa ofisi yake, alitamka kusitisha shughuli za mabaraza hayo.

Hata hivyo, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-Tamisemi, Mussa Iyombe alizungumza na Mwananchi jana kuhusu tamko la Makonda alisema mkuu huyo wa mkoa ameshatoa ufafanuzi kwa maandishi.

Alisema Makonda alikana kuwa hajasimamisha mabaraza hayo kufanya kazi.

“Tulimtaka atuandikie barua ya kutueleza na tayari ameshafanya hivyo, tumemalizana naye kwa maandishi, hakusimamisha mabaraza hayo kufanya kazi,” alisema Iyombe.

Alisema, “Mtapata taarifa mkimuuliza mwenyewe, kwa upande wetu tumemalizana naye.”

Alipotakiwa kusema kama mkuu huyo wa mkoa alitakiwa kuandika barua baada ya kuvunja kipengele kipi cha sheria kutokana na tamko lake Iyombe alisema:

“Sitaki kusema alivunja kipengele ni wewe wasema, ninachosema kama kiongozi lazima unachokisema wananchi wakielewe, kulikuwa na maswali watu wanahoji kuhusu suala hilo ndiyo maana tukamtaka atufafanulie na amefanya hivyo kwa maandishi. ”

Makonda alipotafutwa kuzungumzia suala hilo jana, simu yake ya mkononi iliita bila ya kupokewa.

Wakati Iyombe akisema hayo, Ofisa Mtendaji Kata ya Kigogo, Ole Rosai akizungumzia tamko la Makonda jana alisema, “Mimi nilisikia tu katika vyombo vya habari kwa hiyo nasubiri mwongozo kutoka kwa mkurugenzi kujua utekelezaji wake.”

Kauli ya Rosai iliungwa mkono na Ofisa Mtendaji Kata ya Ubungo, Isack Waziri aliyesema bado hawaelewi utekelezaji wake.

“Ni kweli lazima tupate maelekezo rasmi ya kimaandishi lakini kama bosi wako amesema unafanyaje? Tumewasiliana na mwanasheria wa manispaa (ya Ubungo) katueleza analifuatilia,” alisema Waziri.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Temeke, Nassib Mmbaga alisema, “Hili jambo si limetokea juzi, ili litekelezwe linahitaji kuandikiwa barua lakini kwa sasa na sisi tunasubiri maelekezo kutoka kwa Katibu Tawala Mkoa kuwa linatekelezwa hivi na hivi. Kwa hiyo tunasubiri.”

Katibu Tawala Mkoa wa Dar es Salaam, Theresia Mmbando hakupatikana kuzungumzia tamko hilo.

Meya wa Ubungo, Boniface Jacob alisema, “Serikali haifanyi kazi kwa kauli za WhatsApp au redio. Maelekezo tunapata kutoka kwa katibu mkuu Tamisemi.”

Jacob ambaye pia ni Diwani wa Ubungo alisema, “Hata Rais anapotoa maelekezo huwa baadaye yanaambatana na barua.”

Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula alipoulizwa na Mwananchi kuhusu kusimamishwa kwa mabaraza hayo alisema, “Hayo wasiliana na Waziri wa Tamisemi, hayako katika wizara yangu. Tamisemi ndiyo yanawahusu.”

Rais wa zamani wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS), Felix Kibodya akizungumza na Mwananchi juzi alisema mabaraza hayo yalianzishwa mwaka 1985 ili kushughulikia migogoro ya ardhi na halmashauri zilipewa jukumu la kuyasimamia.

Alisema mabaraza hayo yaliongezewa nguvu zaidi kwenye Sheria ya ardhi ya Kijiji ya mwaka 1999 na Sheria ya Utatuzi wa Migogoro ya mwaka 2002.

Kibodya alisema haiwezekani mabaraza hayo kusimamishwa kufanya shughuli zake kwa kuwa mambo ya kisheria hayawezi kuondolewa kwa matamko ya jukwaani.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad