Beki wa Kagera Sugar, Juma Nyoso amefungiwa kucheza michezo mitano ya Ligi Kuu Tanzania Bara sambamba na faini ya Sh1 miolioni kwa kosa la utovu wa nidhamu.
Akifafanua adhabu hiyo, msemaji wa TFF, Clifford Mario Ndimbo amesema beki huyo amekutwa na hatia ya kumpiga shabiki mara baada ya mchezo dhidi ya Simba kumalizika.
"Kamati ya nidhamu ilimuita Nyoso ili kujitetea kama ilivyo kawaida lakini kwa upande wake alikana kuhusika na tukio hilo na badala yake akadai alimkunja shabiki huyo.
"Lakini ripoti ya mchezo huo kutoka kwa mechi kamishina imeeleza kuwa Nyoso alimpiga shabiki huyo kwa kiatu na kisha akatumia goti," alisema Ndimbo.
Hata hivyo adhabu hiyo imetajwa kutolewa kwa kanuni ya 36 ya Ligi Kuu inayohusu uchezaji wa kiungwana, kipengele cha (1),(2) na (5).
Pia kamati ilirejea aina ya matukio ya utovu wa kinidhamu ambayo amewahi kuyafanya beki huyo ambaye amewahi pia kuichezea Taifa Stars na klabu ya Mbeya City.