Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu imemsomea maelezo ya awali mkurugenzi mkuu wa
zamani wa Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC), Tido Mhando
anayekabiliwa na mashtaka matano likiwamo la matumizi mabaya ya
madaraka.
Kabla
ya kusomewa maelezo leo Februari 28,2018 mbele ya Hakimu Mfawidhi,
Victoria Nongwa, Wakili wa Serikali Dismas Mganyizi, alimkumbusha
mashtaka yanayomkabili Tido anayetetewa na wakili Ramadhani Maleta.
Baada
ya kusomewa, Tido ambaye yuko nje kwa dhamana amekubali maelezo binafsi
na kwamba alikuwa mkurugenzi mkuu wa TBC mwaka 2006 hadi 2010.
Amekubali kuwa alikuwa msimamizi wa shughuli za TBC lakini si zote.
Pia
amekubali kutoa maelezo kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa
(Takukuru) na kuwa alifikishwa mahakamani Januari 26,2018.
Tido amekana mashtaka yanayomkabili na upande wa mashtaka katika kesi hiyo utaanza kutoa ushahidi Machi 28,2018.
Anakabiliwa na mashtaka manne ya kutumia madaraka vibaya na moja la kuisababishia Serikali hasara ya Sh887.1 milioni.
Tido
anadaiwa Juni 16,2008 akiwa Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE),
akiwa mkurugenzi mkuu wa TBC kwa makusudi alitumia madaraka yake vibaya
kwa kusaini mkataba wa kuendesha na kutangaza vipindi vya televisheni
kati ya TBC na Channel 2 Group Corporation (BV1) bila kupitisha zabuni
kinyume cha sheria ya ununuzi, hivyo kuinufaisha BVl.
Katika
shtaka la pili anadaiwa kutumia vibaya madaraka yake ikielezwa Juni
20,2008 alisaini makubaliano ya utangazaji wa digitali duniani kati ya
TBC na BVl.
Tido
katika shtaka la tatu anadaiwa Agosti 11,2008 na Septemba 2008 akiwa
Dubai alitumia vibaya madaraka yake kusaini mkataba wa makubaliano ya
ununuzi, usambazaji, kufunga vifaa vya usambazaji na mnara wa utangazaji
kati ya TBC na BVI na kuifaidisha BVI.
Shtaka
la nne, anadaiwa Novemba 16,2008 akiwa Dubai alitumia vibaya madaraka
yake kusaini mkataba wa makubaliano ya kuendesha miundombinu ya
utangazaji kati ya TBC na BVI na kuinufaisha BVI.
Tido katika shtaka la tano anadaiwa kati ya Juni 16 na Novemba 16,2008 akiwa Dubai aliisababishia TBC hasara ya Sh887.1 milioni.